Habari za Punde

UWAJIBIKAJI NDIO SIRI YA MAFANIKIO CHINA - BALOZI MAPURI

Ramadhan Makame, Beijing

BALOZI wa Tanzania nchini China, Omar Ramadhan Mapuri amesema siri ya maendeleo ya haraka yaliyofikiwa na China inatokana na uwajibikaji, nidhamu na kujituma.

Balozi Mapuri alieleza hayo mjini Beijing kwenye hafla fupi iliyofanyika katika ukumbi wa Ubalozi huo, ambapo alikutana na ujumbe wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ulio kwenye mafunzo ya wiki mbili nchini humo.


Alisema China imepiga hatua kubwa za maendeleo na ya haraka na itazidi kuendelea zaidi kwani viongozi na wananchi wa nchi hiyo ni wenye kujali uwajibikaji katika utekelezaji wa mipango yao.

Aidha alisema sababu nyengine iliyoharakisha maendeleo yaliyofikiwa hivi sasa na taifa hilo, ni nidhamu pamoja na kujituma.

“Sina haja ya kueleza siri ya maendeleo ya China naamini mmejionea wenyewe, lakini kitu cha muhimu ni kwamba wenzetu ni wawajibikaji, wananidhamu ya utekelezaji na pia ni watu wenye kujituma”,alisema Balozi Mapuri.

Alifahamisha kuwa China kabla ya kufikia maendeleo iliyokuwa nayo hivi sasa ilikaa chini na kusomesha vijana wake katika nchi mbali mbali za Magharibi ambao hivi leo ndio wanaotumika kulijenga taifa hilo.

Aidha Balozi huyo alisema utulivu wa kisiasa uliofikiwa visiwani Zanzibar umefuta masuali magumu ambayo mabalozi mbali mbali wa Tanzania walikuwa wakikumbana nayo.

“Hivi sasa tunapokutana na wenzetu wa huku nje, yale masuali magumu ambayo tulikuwa tukiulizwa kuhusu hali ya siasa ya Zanzibar sasa hayapo”, alisema Balozi huyo.

Alifahamisha kuwa badala ya kuuliza masuali hayo hivi sasa wamekuwa wakipongeza kutokana na kutengemaa hali ya siasa ya Zanzibar iliyotokana na uundwaji wa serikali ya Umoja wa kitaifa.

Akizungumzia uhusiano wa China na Tanzania, Balozi Mapuri alisema zipo nchi zimekuwa zikiionea wivu Tanzania jinsi inavyofaidika na misaada mingi ikilinganishwa na wao na hata kudai imekuwa ikipendelewa.

“Ushirikiano kati yetu na China ni mkubwa mno, imefikia wakati hata baadhi ya nchi za wenzetu zimekuwa zikilia uteka kama sisi tunapendelewa zaidi”, alisema Balozi huyo.

Kwa upande wake akitoa neno la shukurani kwa niaba ya uongozi wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, waziri wa Katiba na Sheria wa Zanzibar, Aboubakar Khamis Bakary, alisema ujenzi mpya wa siasa za Zanzibar umelenga kuwaunganisha wananchi ili waweze kufikia maendeleo.

Alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Umoja wa kitaifa imeweka kipaumbele cha kukuza na kuendeleza maisha ya wananchi.

Ujumbe wa serikali ya Mapinduzi katika hafla hiyo rasmi uliongozwa na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho.

Ujumbe huo wenye mawaziri kadhaa Naibu waziri na watendaji wa serikali uliondoka Beijing jana na kuelekea mji wa Suzhou na baadae Shanghai, kabla ya kumaliza mafunzo na kurejea nyumbani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.