Habari za Punde

ZANZIBAR HEROES YASUBIRI MANUSRA YA WAGANDA

Mwandishi Wetu

UHAI wa timu ya Zanzibar kusonga mbele katika Michuano ya Tusker Chalenji utategemea manusura ya Uganda endapo itaifunga Burundi katika mchezo wa pili wa Kundi B la michuano hiyo kwenye Uwanja wa Taifa.

Kimahesabu, Zanzibar yenye pointi moja baada ya sare ya Burundi na ilifungwa mchezo wa kwanza na Uganda mabao 2-1 inacheza na Somalia na inatakiwa kuifunga timu hiyo mabao yasiyopungua manne.Uganda inayoongoza Kundi B ikiwa na pointi sita, iliifunga Somalia mabao 4-0, mechi iliyopigwa Chamazi pamoja na Zanzibar 2-1 katika mechi ya kwanza.


Sasa Zanzibar inachohitaji, Uganda iifunge Burundi idadi yoyote ya mabao bila majibu na yenyeweiifyeke Somalia idadi hiyo ya mabao yasiyopungua manne. Sare ya Uganda na Burundi itakuwa imeiondosha Zanzibar mashindanoni.

Zanzibar ina pointi moja na ikishinda itakuwa na pointi nne sawa na Burundi na kitakachokuwa kinaangaliwa ni mabao ya kufunga na kufungwa na endapo matokeo yatasimama hivyo, Zanzibar itakuwa imefuzu na kuiacha Burundi ikirudi nyumbani kwani itakuwa imeizidi kwa mabao ya kufunga.

Hali hiyo inatokana na Zanzibar kuboronga katika mechi zake mbili ikiwemo moja ya suluhu na Burundi. Mechi zote za leo, zitachezwa kwenye Uwanja wa Taifa.

Naye Calvin Kiwia anaripoti kuwa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars imeibandua Ethiopia mabao 2-0 katika mchezo mkali kwenye Uwanja wa Taifa.Matokeo hayo yamefufua matumaini ya timu hiyo ambayo ililazwa mabao kama hayo na Malawi katika mchezo wa kwanza.

Mabao ya washindi yalikwekwa kimiani na Bob Mugaria katika dakika ya 11 wakati bao la pili lilifungwa na Victor Ochieng dakika tatu kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika.Katika mchezo mwingine, Malawi na Sudan zimetoka suluhu ikiwa ni mfululizo wa michuano hiyo kwenye uwanja huo.

Wakati huo huo, Imani Makongoro anaripoti kuwa mshambuliaji wa Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars Mbwana Samatta ameondolewa kwenye kikosi cha timu hiyo baada ya kuumia enka na hatoweza kucheza tena.

Samatta aliumia katika mechi ya kwanza ya Kilimanjaro Stars dhidi ya Rwanda “Amavubi” na daktari alimpa siku 10 za kupumzika bila ya kufanya mazoezi ya aina yoyote kwa mujibu wa kocha mkuu wa timu hiyo, Charles Boniface Mkwasa.

Mkwasa alisema kuwa mshambuliaji huyo wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amekwisha ondoka kambini kwa ajili ya kujiuguza na wao wameshindwa kuziba pengo lake kutokana na ukweli kuwa amekwisha cheza mechi moja.

CHANZO : Mwananchi

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.