Ni baada ya kuitafuna Somalia, Burundi yaichapa Uganda
Na Salum Vuai, Dar es Salaam
TIMU ya taifa ya soka Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’, jana ilijisogeza karibu na robo fainali ya michuano ya ‘Tusker Challenge Cup’, baada ya kuitafuna Somalia mabao 3-0, katika mchezo wake wa mwisho uliopigwa katika uwanja wa Taifa jijini hapa.
Hata hivyo, kutinga kwake katika hatua hiyo, kutategemea hesabu za timu nyengine kwa kuangalia washindwa bora.
Zanzibar ilianza mchezo huo kwa kasi, ikionesha dhamira ya kusaka magoli mengi mapema na kufanikiwa kuandika goli la kwanza mnamo dakika ya tisa kupitia kwa Suleiman Kassim ‘Selembe’, aliyeunganisha kwa shuti krosi iliyochongwa na Abdallah Seif ‘Amorosso’.
Kufuatia goli hilo, Zanzibar iliyokuwa chini ya makocha Hemed Suleiman ‘Moroko’ na Stewart John Hall aliyerudi kikosini baada ya hivi karibuni kutangaza kuachia ngazi, ililiandama lango la Wasomali na kuwaweka walinzi wake katika wakati mgumu.
Hata hivyo, licha ya mashambulizi mengi waliyofanya langoni mwa timu hiyo, Zanzibar Heroes ilishindwa kuongeza bao la pili na kulazimika kwenda mapumziko wakiongoza 1-0.
Somalia iliyocheza kichovu katika kipindi cha kwanza, ilianza ngwe ya pili kwa kubadilisha mchezo, huku kocha wake Mkenya Alfred Imonja, akijaribu kuwahamasisha ili kuzifikia nyavu na kuwazuia Heroes wasiongeze magoli.
Katika dakika ya 47, mchezaji Mohammed Osman wa Somalia, alimjaribu mlinda mlango Mwadini Ali kwa shuti la nguvu, lakini liliishia mikononi mwa golikipa huyo.
Zanzibar ilicharuka na kumudu kuzifumania nyavu kwa mara ya pili, ambapo Amir Hamad baada ya wachezaji wa timu hiyo kugongeana vyema mpira, ambao awali ulitemwa na mlinda mlango Khalid Ali kabla mfungaji huyo kuukwanmisha wavuni.
Kufuatia bao hilo, washambuliaji wa Zanzibar Heroes walihamia langoni mwa Uganda, ambapo mashuti mengi yaliokolewa au kutoka nje na kuwanyima mabao mengi zaidi.
Kwa dakika kadhaa, Somalia walipata uhai na kugongeana vizuri lakini walishindwa kulenga lango, kabla kujikuta wakipachikwa bao la tatu katika dakika ya 85 lililofungwa na mlinzi Aggrey Morris aliyeruka kuunganisha kwa kichwa mpira wa kona uliochongwa upande wa mashariki ya uwanja.
Nayo Burundi imeweza kushika uongozi wa kundi hilo baada ya kuibanjua Uganda kwa bapo 1-0 katika mchezo uliochezwa majira ya saa 10:00 jioni, na kujikusanyia pointi saba huku Uganda Cranes ikishika nafasi ya pili kwa pointi sita, na kuzifanya timu zote hizo kutinga robo fainali.
Michuano hiyo inaendelea tena leo kwa mechi ya kundi A ambapo wakati wa saa 8:00 mchana, Rwanda itakamilisha ratiba kwa kuivaa Djibouti iliyokwishaaga, huku Ethiopia na Malawi zikitiana mbavuni mnamo saa 10:00 jioni ukiwa mchezo wa kundi C
No comments:
Post a Comment