Habari za Punde

Kima cha Chini Sekta Binafsi Kutangazwa

Na Mwantanga Ame

SERIKALI ya Zanzibar ikiingia katika mwaka mpya wakati wowote inatarajiwa kutangaza kupandisha mshahara kwa wafanyakazi katika sekta binafsi.

Ali Salum Ali, Katibu wa vyama vya wafanyakazi aliyasema hayo hivi karibuni wakati akizugumza na vyombo vya habari vya hapa nchini.


Katibu huyo alisema hatua hiyo serikali itaichukua baada ya kumalizika kwa mazungumzo na wadau wa sekta binafsi na serikali juu ya kuangalia maslahi ya wafanyakazi katika eneo hilo.

Katibu huyo alisema, wameamua kuchukua hatua hiyo ikiwa ni sehemu ya taratibu za kuwajali watumishi katika sekta binafsi ambao ndio wadau wao wakuu.

Alisema katika kipindi cha miaka mitatu walishindwa kufanya mabadiliko ya mishahara katika sekta hiyo kutokana na Bodi ya mishahara ya sekta binafsi kushindwa kukaa.

Hali hiyo alisema ilikuja kutokana na kupisha kufanyika utafiti wa utumishi katika sekta hiyo uliofanyika mwaka 2010.

Alisema kutokana na hali hiyo hivi sasa serikali imeamua kukaa pamoja na wadau wa sekta binafsi ikiwa pamoja na kuamua mambo ya msingi yanayohusu sekta binafsi kwa kuzingatia na hali ya uchumi hapa nchini.

Alisema katika kikao hicho tayari kuna mapendekezo ambayo yametolewa na wadau hao ya kupandisha kima cha mshahara kwa sekta hiyo ambayo baadae yatayowasilishwa serikalini ili waweze kuyatolea maamuzi.

Alisema yeye binafsi hataweza kutoa mapendekezo ya viwango vilivyoamuliwa na kikao hicho kwa vile kazi hiyo itatangazwa rasmi na Waziri wa Wizara ya Kazi Uwezeshaji Wananchi na Ushirika.

Akizungumzia juu ya baadhi ya Waajiri katika sekta binafsi katibu huyo alisema kumekuwa na baadhi ya waajiri kushindwa kutoa ushirikiano na vyama vya Wafanyakazi pale wanapotakiwa kutoa taarifa sahihi hasa
zinazohusu maslahi ya wafanyakazi.

Akitoa mfano Katibu huyo alisema hivi sasa kuna baadhi ya wamiliki wa taasisi hasa katika mahoteli wamekuwa wanashindwa kuwachangiawatumishi wao fedha za mfuko wa hifadhi ya Jamii huku wakiwa hawatoi taarifa sahihi.

Kutokana na hali hiyo tayari hivi sasa Chama cha Wafanyakazi Mahotelini kimeanzisha utaratibu wa mazungumzo na taasisi hizo kujuwa wajibi wa kutekeleza sheria hiyo.

Akizungumza na Zanzibar Leo Waziri wa Wizara ya Kazi Uwezeshaji Wananchi na Ushirika Haroun Ali Suleiman, alithibitisha kuwa serikali ina nia ya kupandisha mshahara kwa sekta binafsi.

Alisema hivi sasa wanajiandaa kufanya mapitio mbali mbali ili kuweza kuweka mambo sawa ambapo Ijumatano wanatarajia kutangaza rasmi viwangovipya vya mishahara hiyo.

Waziri huyo, alisema viwango vipya vya mshahara kwa sekta hiyo vinatarajiwa kupanda kwa asilimia 20 ambapo kiwango cha sasa cha kima cha chini kwa sekta binafsi kimefikia shilingi 30,000.

Alisema katika viwango vipya serikali pia itapandisha mishara ya wafanyakazi wa majumbani na maeneo mengine.

“Ni kweli tunajiandaa kupandisha mishahara ya sekta binafsi na Ijumatano natarajia kuwa tutaitangaza rasmi kwani hivi sasa kuna mambo mengi bado hatujesha kuyaangalia lakini hilo lipo na tumo katika hatua
ya kulimaliza” ,alisema Waziri huyo.

Taarifa za kupanda kwa mishahara kwa sekta binafsi tayari watumishi wa kada hiyo wameonekana kuwa na shauku kubwa kujua kiasi ambacho wataweza kupandishiwa mishahara yao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.