Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na wajumbe wa kamati ya mfuko wa maendeleo ya watu wenye ulemavu katika uzinduzi wa mfuko huo uliofanyika ofisini kwake Migombani. Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe. Fatma Abdulhabib Fereji na kushoto ni mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Nassor Ahmed Mazrui.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa kamati ya mfuko wa maendeleo ya watu wenye ulemavu mara baada ya kuizindua kamati hiyo huko Ofisni kwake Migombani.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema wakati umefika wa kuwakomboa watu wenye ulemavu na kuwasaidia ili waweze kuishi kwa kufurahia haki zao za msingi kama walivyo watu wengine.
Amesema kwa muda mrefu jamii imekuwa ikiwatenga na kuwakosesha haki zao za msingi zikiwemo huduma za afya na elimu, jambo ambalo linapaswa kupigwa vita katika jamii ya sasa.
“tukumbuke kuwa hawa na ni watu kama sisi, nasi sote ni walemavu watarajiwa, kwa nini tunawatenga na kuwakosesha haki zao”? alihoji Maalim Seif.
Maalim Seif ameeleza hayo huko ofisini kwake migombani mjini Zanzibar alipokuwa akizindua kamati ya mfuko wa maendeleo kwa watu wenye ulemavu wa aina mbali mbali.
Amepongeza hatua ya serikali kupitia Wizara ya elimu na Mafunzo ya Amali kwa kuanzisha elimu mjumuisho ambayo inatoa fursa sawa ya elimu kwa watu wote wakiwemo wenye ulemavu.
Makamu wa Kwanza wa Rais ameitaka kamati hiyo kufanya juhudi za maksudi ili kutunisha mfuko huo wenye lengo la kuwasaidia na kuwaendeleza watu wenye ulemavu hapa Zanzibar.
Mapema akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wan chi, ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe. Fatma Abdulhabib Fereji amesema Wizara yake inaendelea na sensa ya kuwatambua watu wenye ulemavu ambapo kwa sasa tayari imekamisha kazi hiyo kwa mikoa mitatu.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuwatambua watu hao na maeneo wanayoishi, kwa lengo la kuwasogozea huduma zinazostahiki, na kwamba sula la watu wenye ulemavu ni zito na halipaswi kupuuzwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, ameiasa jamii kuacha vitendo vya ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu na kuahidi kushirikiana na wajumbe wa kamati hiyo kuutunisha mfuko huo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Kamati hiyo yenye wajumbe tisa, inaongozwa na Mhe. Nassor Ahmed Mazrui (Mwenyekiti), Mhe. Abdallah Mwinyi Khamis (Makamu Mwenyekiti) na Bi Fauzia Haji Mwita (Katibu).
No comments:
Post a Comment