Wa Mamlaka Usafiri baharini aachishwa kazi
Na Mwantanga Ame
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kivitendo kukubaliana na ripoti ya Tume ya Rais ya kuzama kwa meli ya Mv. Spice Islanders kwa kuwawajibisha waliotajwa kuzembea kutokana na ajali hiyo.
Kutokana na hali hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari, Mustafa Aboud Jumbe, amehamishwa kwenye shirika hilo aliloliongoza kwa miaka kadhaa ambapo amehamishiwa katika Idara ya Miundombinu.
Ripoti hiyo iliyotolewa hivi karibuni mbele ya waandishi wa habari na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, ilimtaja Mkurugenzi huyo kuwa ni miongoni mwa walioshindwa kuwasimamia vyema wafanyakazi wake wa kada za chini.
Aidha Mkurugenzi huyo alitajwa kwenye ripoti hiyo kuwa alishindwa kudhibiti usalama wa bandari na wa vyombo vya usafiri wa baharini kwa kuruhusu utaratibu mbovu wa abiria kuingia bandarini na kwenye meli
hali hali iliyochangia kuuzwa tiketi chini ya ngazi ya kuingilia melini na pia watu kupenyezwa melini bila ya kuwa na tiketi.
Tuhuma nyengine kwa mujibu wa ripoti ya Tume hiyo ni kushindwa kudhibiti usalama wa vyombo kwa kuruhusu utaratibu wa vyombo kuingiza abiria na kupakia mizigo kwa wakati mmoja, pamoja na kushindwa
kudhibiti usalama wa bandari kwa kuruhusu wachukuzi kuingia bandarini na kufanya kazi bila ya kuwa na sare.
Mambo hayo yametajwa kuwachangia kutokea kwa ajali hiyo iliyopoteza roho za watu 203 mwezi Setemba mwaka jana.
Katika mapendekezo ya ripoti hiyo Mustafa, ilitajwa angepaswa kuchukuliwa hatua za kinidhamu kutokana na kutohusika moja kwa moja kuzama kwa meli hiyo.
Akizungumza na gazeti hili, Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu, Hamad Masoud Hamad, alithibitisha kuhamishwa kwa Mkurugenzi huyo na kupokea barua uhamisho huo na kwamba ataripoti katika Idara yake mpya ya Miundombinu.
Alisema haijajulikana nafasi atayoshika katika Idara hiyo mpya kwa vile uhamisho wake haujaeleza lolote zaidi ya kuhamishwa kuripoti Idara ya Miundombinu.
“Ni kweli nimepokea barua yake ya uhamisho na tayari tumeshamjulisha juu ya maamuzi ya serikali, baada ya ripoti ya Mv. Spice kutolewa”, alisema waziri huyo.
Aidha alieleza kuwa katika kuwachukulia hatua watu waliotajwa ambao wamo ndani ya utumishi wa wizara hiyo, alisema ni pamoja na Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Usafiri baharini, Injinia Haji Vuai Ussi, ambaye
ameachishwa kazi baada ya ripoti hiyo kumtaja kuwa ni miongoni mwa waliozembea.
Waziri huyo, alisema tayari Mkurugenzi huyo ameshapatiwa barua yake kuarifiwa kuwa ameachishwa kazi.
Mkugenzi huyo wa zamani wa shirika la Banadari ameondolewa kuliongoza shirika hilo akiwa kwenye madaraka hayo tangu utawala wa Rais wa Awamu ya tano, Dk. Salmin Amour na Utawala wa Rais Mstaafu, Dk. Amani Abeid Karume.
Itakumbukwa kuwa hapo juzi Spika wa Baraza la Wawakilishi alitoa taarifa katika baraza hilo kuwajuulisha wajumbe kuwa mmoja wa wajumbe wake, alikamatwa na polisi akihusishwa na kuzama kwa meli hiyo.
Spika Kificho alimtaja Mwakilishi huyo kuwa ni Jaku Hashim Ayoub kutoka Jimbo la Muyuni, ambapo baada ya kushikiliwa na Polisi alihojiwa na kuachiliwa kwa dhamana.
Mwakilishi huyo alitajwa kwenye ripoti huyo ni mwanahisa katika umiliki wa meli ya Mv. Spice Islanders kutoka kampuni ya Al-qubra ambapo waliiruhusu meli yao ifanye kazi hali wakijua ina matatizo ya kiufundi, pamoja na kutokuwa na mabaharia wenye sifa.
Aidha mwishoni mwa wiki iliyopita watu zaidi ya 10 walifikishwa katika Mahakama Kuu Zanzibar wakihusishwa kuzembea hadi kuzama kwa meli hiyo iliyokuwa ikitokea Unguja kuelekea Pemba.
Wakati akiwasilisha ripoti Katibu Mkuu Kiongozi alisema serikali imekubaliana na mapendekezo ya ripoti hiyo na itawachukulia hatua za kisheria na kinidhamu wote waliotajwa ndani ya ripoti hiyo na wataohitajika kushughulikiwa kisheria vitaachiwa vyombo vya sheria.
Great. Kwa kweli si vizuri kumuombea mabaya mwenzio lakinj Mustafa Jumbe alijiona Mungu mtu.
ReplyDeleteNi heri apumzike miaka alodhalilisha wafanyakzi wake inamtosha kuondoka ili watu wapumzike na kiburi chake
Ahsante sana kaka,
ReplyDeletekwa maoni yangu mimi nasema Serikali haikumtendea haki injinia kwa kumfukuza kazi, kama ni uzembe na Mustapha pia anahusika kikamilifu kama ripoti yenyewe ilivoeleza au kwa kuwa ni mtoto wa Jumbe???
Kwakweli inatia moyo, ni uamuzi mzito ambao kwa siku za nyuma kidogo tu usinge weza kuchukuliwa.
ReplyDeleteNa kama tutaendelea hivi, huenda tukaondokana ile 'culture of impunity'(utamaduni wa kushindwa kuwajibishana).
Ama kuhusu madai kwamba, injinia amefukuzwa kazi na Mustafa amebadilishawa kituo cha kazi huenda kwa vile ni mtoto wa Jumbe.. hivi vitu havihusiani!
Serikali haiwezi kufanya upuuzi wa namna hiyo. Huwenda wameangalia viwango vya uhusika wa kila mmoja na mapendekezo ya tume.
Hizo ndio gharama za utawala bora na uwajibikaji tunazozihubiri kila siku, inauma lakini inabidi.
Ama mimi kwa upande wangu bado nalia na waziri wa miundo mbinu..najiuliza kwa nini asijiuzulu kupitia 'Ministerial responsibility'
kwa makosa yaliyotendwa na watendaji walio chini yake?..leo hii bado anaonekana anacheka cheka kwenye hafla mbali mbali!
Alipokua nje ya serikali alikua na maneno mabaya kama nini..dhidi ya wenzake..na yeye kaja kufanya yaleyale..alitakiwa ajue 'uongozi si lelemama'