Habari za Punde

Wawakilishi: Mswada wa Rushwa Utekelezaji Ahadi za Dk.Shein

Washauri kuundwa Kitengo cha maadili ya viongozi

Na Mwantanga Ame

WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wamesema baada serikali kusaini sheria ya Rushwa, ni vyema ikaunda kitengo cha maadili ya viongozi ili kuwazesha kutaja mali zao na watakuwa tayari kumbainishia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, viongozi wala rushwa.

Wajumbe hao waliyasema hayo jana wakati wakichangia mswada wa sheria ya uundwaji wa Mamlaka ya Rushwa katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachofanyika nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haji Omar Kheir, akiwasilisha mswada huo alisema sheria hiyo kutaondoa shughuli za kufuatilia matendo ya rushwa katika Jeshi la Polisi, na sasa kazi hizo zitafanyika katika chombo husika.

Alisema chombo hicho kitakuwa kinajitegemea chenyewe na hakitakuwa na kazi ya kuchunguza matukio ya rushwa pekee bali pia kitafanya kazi ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matatizo na madhara ya rushwa na
majukumu mengine.

Kheir alibainisha makosa mbali mbali ndani ya sheria hiyo, pamoja na adhabu zitazotolewa kwa wataotiwa hatiani.

Wawakilishi hao walisema serikali baada ya kuipitisha sheria hiyo ni vyema ikaunda kitengo hicho kwa lengo kuiwezesha serikali kupima uwazi wa uwajibikaji na watakuwa tayari kumsaidia Rais kwa kuwapelekea watu
wanaotajwa kula rushwa.

Walisema vitendo vya rushwa hivi sasa vimeonekana kuenea kutokea katika maeneo mengi jambo ambalo limekuwa likiwapunguzia wananchi imani na utendaji wa shughuli za serikali.

Wajumbe hao walisema ikiwa serikali itaweka kitengo hicho kwa kiasi kikubwa kitawawezesha wananchi kuwa na imani na viongozi wao kwa vile wataweza kutambulika mali zao na hali za maisha yao.

Walisema baadhi ya viongozi na watendaji katika taasisi za serikali wamekuwa wakionekana wanapoingia madarakani wakiwa hawana mali nyingi, lakini baada ya kipindi kifupi huwa ni wenye kumiliki kiasi kikubwa
cha mali ambacho hakilingani na kipato wanacholipwa.

Mwakilishi wa Chake chake, Omar Ali Shehe, akitoa mchango wake alisema Dk. Shein amefanya jitihada kubwa ya kuharakisha kuandaa mswada wa rushwa baada ya kutambua bila ya kudhibiti hilo linaweza kuleta athari za kiuchumi.

Alisema kuwepo kwa mswada huo ni sehemu itayoimarisha utawala bora na kuweza kurudisha imani kwa wananchi katika ustawi wao wa maisha.

Alisema jambo la msingi ambalo linahitaji kufanyika ni kuwapo kwa tume ya maadili itayowafanya viongozi wa Zanzibar kutaja mali zao ikiwa ni sehemu ya kuimarisha utawala bora.

Mwakilishi wa Kwamtipura, Hamza Hassan Juma, akitoa mchango wake alisema taasisi ya rushwa kwa wanasiasa inaweza ikapata tabu sana hasa katika kipindi cha uchaguzi na itaweza kuwatoa imani wananchi kwa vile baadhi ya viongozi wameonekana kupenda kutumia rushwa kununua uongozi.

Alisema ni vyema kwa serikali kabla ya kuanza kutumika kwa sheria hiyo ikafikiria kuunda Tume ya maadili ya viongozi ili kuweza kuwa na kigezo kizuri cha kuweza kumpima kiongozi asiekula rushwa wala kujilimbikizia mali.

Aidha, alisema hivi sasa kuna taizo kubwa la rushwa katika maeneo ya ardhi inayotokana na utumiaji mbaya wa madaraka ya baadhi ya viongozi likiwemo eneo la mikataba kuonekana kuongoza kwa rushwa.

Alisema hivi sasa rushwa imechangia sana uharibifu wa mazingira katika ujenzi wa mahoteli mengi ya kitalii kutokana na kuruhusu kujengwa karibu na bahari kwa kuthubutu hata kukiuka taratibu za kisheria huku
kukiwa na rushwa iliyokithiri ngono katika ajira za kitalii.

Nae, Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe Ismail Jussa Ladhu, akitoa mchango wake, alisema serikali kuleta sheria hiyo imeweza kutekeleza ahadi yake ya kutaka kupambana na Rushwa Zanzibar.

Hiyo alisema kwa kiasi kikubwa kutaweza kusababisha kuwepo kwa mabadiiko ya watendaji wa serikali na viongozi ili kutekeleza majukumu yao kwa kufuata misingi ya kisheria.

Alisema hivi sasa rushwa katika zabuni imekithiri ambapo baadhi ya ushahidi uliwekwa wazi ndani ya baraza hilo likiwemo wa ukodishwaji wa kisiwa cha Changuu, ukumbi wa Disco wa hoteli ya Bwawani na ununuzi wa mitambo.

Mwakilishi huyo pia aliitaka serikali kuyaangalia baadhi ya Mahoteli ya kitalii kutokana na kukwepa kodi kwani wameanzisha tabia ya kuomba msamaha wa kodi lakini baada ya kupewa misamaha hiyo husafirishwa kwa boti zao binafsi kupeleka Tanzania bara na kuifanya Zanzibar kama ni mlango wa kupitisha vifaa hivyo.

Mwakilishi wa Jimbo la Kitope Makame Mshimba, akichangia mswada huo alisema hivi sasa kumekuwa na tatizo kubwa la baadhi ya viongozi kuonekana kukumbatia vitendo vya rushwa hasa katika Jeshi la Polisi
kwa Mkoa wa Kaskazini na atakuwa tayari kuwabainisha wahusika wa vitendo hivyo mbele ya Rais.

Alisema inasikitisha kuona viongozi wa Jeshi hilo hivi sasa hawafai kwani wamekuwa wakiitumia vibaya mfumo wa Polisi Jamii kwa kuwadhalilisha wananchi.

Nae Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani, Hijja Hassan Hijja, akitoa mchango wake alisema ipo haja kwa Rais apewe mamlaka ya kumuondoa kiongozi yoyote atayekuwa amebainika kula rushwa

Mwakilishi wa Ziwani, Rashid Seif, alisema hivi sasa kumekuwa na tatizo la uuzwaji wa majengo ya serikali yanayoashiria kuwepo mazingira ya rushwa, katika mikataba ya serikali huuzwa yakiwa hayana hata uwezo wa kuinufaisha serikali huku wengine huweka asilimia kubwa ndani ya mikataba serikali inayoifunga kwa faida zao.

Mwakilishi wa Muyuni, Jaku Hashim Ayoub, akitoa mchango wake alisema baadhi ya vifungu vya sheria hivyo vinahitaji kuwa na uwiano sawa katika utekelezaji wake kikiwemo kifungu kinachohusu suala la viongozi
wanaodai rushwa ya ngono.

Mwakilishi wa Chaani, Ussi Jecha akitoa mchango wake alisema sheria hiyo itapopitishwa inaweza kuongeza mahabusu wengi magerezani kutokana na kukithiri kwa vitendo vya rushwa na itahitaji kuona kunakuwa na
usimamizi mzuri wa utelezaji wake.

Hassan Hamad Omar Mwakilishi wa Kojani, akichangia mswada huo alisema tatizo la rushwa linaendelea kuwa kubwa na hivi sasa limeonekana kushamiri hata katika misikiti ambapo baadhi ya waumini wanagombania uongozi ili wadhibiti misaada inayotolewa kwa misikiti.

Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni, Salmin Awadh Salmin, akitoa mchango wake alisema kuja kwa mswada huo utahitaji kuona utekelezaji unakuwa wa hali ya juu hasa katika taasisi za serikali.

Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud, akitoa ufafanuzi wa kisheria juu ya mswada huo alisema hauna haja ya kupunguza madaraka ya sheria nyengine ila unahitaji umakini katika kuitekeleza.

Mapema akiwasilisha maoni ya Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ya Baraza la Wakilishi, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Panya Ali Abdalla, alisema kamati hiyo inaipongeza serikali kwa kuweka adhabu mbali mbali ndani ya sheria hiyo kwa watu wataofanya vitendo vya rushwa ama kosa la kuhujumu uchumi.

Alisema hatua hiyo inaonesha jinsi Zanzibar, inavyoendelea kufuata misingi ya utawala bora kwani kuja kwa sheria hiyo kutaweza kuleta mabadiliko ya usimamizi bora wa uwajibikaji ambayo sehemu kubwa ya
jamii ilikuwa inayahitaji

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.