Habari za Punde

Walimu Watakiwa Kuongeza Bidii na Kutoa Elimu Bora

Na Iddy Haji Maelezo Zanzibar

Wito umetolewa kwa Walimu kuongeza bidii katika kuwapatia elimu iliyo bora Wanafunzi ili kujenga Taifa lenye wasomi wengi wanaoweza kujitegemea hapo baadae.

Wito huo umetolewa na Waziri asiyekuwa na Wizara maalumu Machano Othman Said wakati wa uzinduzi wa jengo la Skuli ya msingi Mtoni Kigomeni ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar 1964.



Waziri huyo amesema Mapinduzi ya Zanzibar yalikuwa na shabaha ya kuondoa misingi yote ya ubaguzi ikiwemo elimu hivyo Walimu hao wanapaswa kulienzi jambo hilo la kuendelea kutoa elimu bora kwa wote

Aidha amewataka wazazi kuhakikisha wanawapelekeka watoto wao skuli kila wanapofikisha umri wa kwenda skuli jambo ambalo litawatia manufaa hapo baadae

Amesema ili lengo la mapinduzi litimie ni jukumu la wazazi kuhakikisha watoto wao wote hawaonekani mitaani badala yake waonekane skulini wakiwa na ari na moyo wa kujifunza

Sambamba na hayo amewakumbusha kuendelea kuwa na moyo wa kutoa michango midodo midogo inayotakiwa skulini hapo ili kuisaidia Serikali yao yenye dhamana kubwa ya kuwapatia maendeleo wananchi wake

Kwa upande wa wanafunzi Waziri Machano aliwataka Wanafunzi wa skuli hiyo kuachana na vitendo vichafu vinavyoweza kuhatarisha maisha yao ikiwemo uvutaji wa madawa ya kulevya ambao ni kichocheo kikubwa cha maambukizi ya virusi vya ukimwi.

Amewataka Wanafunzi kutumia fursa muhimu waliyoipata kuongeza bidii katika masomo yao ambayo ni ufunguo wa maisha yao na siyo kupuuzia na kujihusisha na mambo yaliokuwa hayana faida kwao na jamii kwa ujumla.

Mapema Msoma risala Mwalimu Mussa Ali amesema licha ya kukamilika Jengo hilo lakini bado kuna changamoto zinazoikabili Skuli yao ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vifaa ya maabara na mmong’onyoko wa ardhi katika skuli yao mambo ambayo yanakwaza maendeleo yao

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.