Na Mwantanga Ame
KAMPENI kwa ajili ya Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Uzini zimesogezwambele na Tume ya Uchaguzi Zanzibar, baada ya kuwepo kwa pingamizi ya rufaa iliyowekwa na mgombea wa Chama cha CUF, dhidi ya Mgombea wa Chama cha Mapinduzi Mohammed Raza Dharamsi.
Chama cha Mapinduzi leo kilikuwa kianze kampeni zake kuwania kiti hicho kwa Jimbo la Uzini, ambapo Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk. Amani Abeid Karume, alitarajiwa kuzindua rasmi kampeni hizo katika kijiji cha Bambi.
Kutokana na kuwapo kwa hali hiyo, Tume ya Uchaguzi Zanzibar, imesema kuwa itasogeza mbele kampeni za uchaguzi huo kuanza baada ya kumaliza kusikiliza rufaa hiyo.
Ofisa Uhusiano wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Idrisa Haji Jecha akizungumza na vyombo vya habari juu ya suala hilo alisema Tume hiyo imelazimika kuzuiya kuanza kwa kampeni za uchaguzi huo baada ya kuwapo
kwa rufaa iliyokatwa na mgombea wa CUF.
Alisema wamelazimika kuzuia kampeni hizo kuanza ili kupisha taratibu
za kisheria kupita baada ya Mgombea wa CUF kukata rufaa kupinga
maamuzi ya pingamizi waliyoiwasilisha katika Afisi ya Tume ya Uchaguzi
ya wilaya.
Alisema mgombea wa Chama cha CHADEMA Ali Mbarouk Mshimba na Mgombea wa
CUF, waliweka pingamizi ya kukipinga kiapo cha Mohammed Raza kwa kudai
kimeshindwa kukidhi matakwa ya kisheria.
Alisema madai mengine alitoa ndani ya waraka wake huo ni kwamba kiapo cha muombaji kimeliwa kinyume cha sheria za viapo Zanzibar (Laws and Decree), pamoja na kukosa stempu halali na ni kinyume na matakwa ya sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Namba 11 ya mwaka 1984 pamoja na
marekebisho yake, kifungu 46 (3) (a).
Akiendelea alisema madai mengine ambayo yametolewa na Mgombea huyo, katika barua yake hiyo ni pamoja na kupinga kiapo cha muombaji kudai kimekosa sifa kwa mujibu wa Sheria ya uchaguzi ya Zanzibar namba 11 ya
mwaka 1984, (3) (a).
Alisema Mlaji kiapo alitakiwa aape mbele ya Hakimu kwa mujibu wa kifungu alichokitaja kwenye aya hiyo, badala yake Raza alikula kiapo aidha mbele ya Jaji au ameghushi muhuri wa Mahakama Kuu.
Ikiendelea hati hiyo ya kumpinga Mwakilishi huyo Mussa, alisema imedai Mlaji kiapo hakuweza kufuata utaratibu wa kisheria ambapo alitakiwa ale kiapo mbele ya Hakimu, na badala yake alikiuka utaratibu huo na
kwa vyovyote vile kiapo hicho hakiwezi kukidhi matakwa ya kisheria kwa kuwa kinapingana na Sheria za Viapo na Sheria ya Uchaguzi Zanzibar.
Kutokana na madai hayo alisema Mgombea wa CHADEMA alieleza kuwa pingamizi walizozieleza hapo juu kutoka kwenye aya ya 1, 2, 3, na 4 na kwa mujibu wa Kifungu namba 46 (4) anamuomba Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Uzini autengue Uteuzi wa Mohammedraza Hassanali Mohamedali, kuwa ni Mgombea halali, na kumuondoa katika orodha ya wagombea waUwakilishi Jimbo la Uzini katika uchaguzi mdogo, kwa kuwa hakuweza kutimiza sifa za kuwa mgombea kwa mujibu wa sheria.
Kutokana na hoja hizo Jecha, alisema Msimamizi wa Uchaguzi wa Wilaya amezitupilia mbali hoja za pingamizi hiyo, baada ya kuridhika kuwa mgombea huyo alifuata sheria za Tume baada ya kuthibitisha kiapo chake
hakikuwa na tatizo.
Maamuzi hayo Jecha alisema Mgombea wa CUF hakukubaliana nayo na kuamua kukata rufaa Tume ya Uchaguzi ambapo inatarajia kukaa Jumapili kupitia Rufaa hiyo na kutoa maamuzi yake.
Alisema hadi hivi sasa ni rufaa moja tu ya mgombea wa CUF, ndio iliyowasilishwa katika Afisi za Tume Wilaya ingawa CHADEMA walishiriki katika kuweka pingamizi hapo awali.
Kutokana na hali hiyo, Jecha alisema kiutaratibu Tume italazimika kuisikiliza rufaa hiyo baada ya kupita masaa 48, tangu Msimamizi wa uchaguzi wa Wilaya kupokea pingamizi hiyo ambapo kwa leo inatarajiwa kumaliza muda wake kuanzia saa 10.00 jioni.
Alisema baada ya kumaliza muda huo Msimamiazi huyo anatarajiwa leo akaiwasilisha rufaa hiyo ambapo Tume itaitolea uamuzi kuanzia saa 8.00 za mchana kesho baada ya kumaliza kikao chake.
Kutokana na hali hiyo Jecha alisema ZEC imelazimika kuzuiya kuanza kwa kampeni hizo hadi shauri hilo litapopata ufumbuzi ikiwa ni hatua ya kuwapa haki sawa wagombea hao kuweza kuanza kufanya kazi hiyo.
Katibu wa CCM Wilaya ya Kati Shukuru Ali, alisema CCM haitaanzakampeni zake leo kwa kusubiri shauri lililofunguliwa na vyama hivyo dhidi ya mgombea wa Chama hicho limalizike.
Alisema wanachama wa CCM wa Jimbo hilo waendeleee kuvuta subira kupisha maamuzi ya rufaa hiyo yafanyike lakini bado wanaimani kubwa mgombea wa CCM ataweza kupangua rufaa hiyo.
Akiakhirisha Mkutano wa Sita wa Kikao cha nne cha Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amewataka wananchi wa Jimbo la Uzini na wanachama wa vyama vya siasa kutumia haki yao kikatiba kupiga kura kwa amani ili kudumisha amani iliyopo nchini.
Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Uzini umepangwa kufanyika Febuari 12, 2012 ambapo Vyama vitatu vinashiriki .
No comments:
Post a Comment