Habari za Punde

Dk Shein Aiasa Wizara ya Elimu Kufufua Michezo Maskuli

Na Rajab Mkasaba, Ikulu

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dr Ali Mohamed Shein, ameeleza haja kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kufufua michezo katika skuli zake kama ilivyokuwa hapo siku za nyuma kwani huko ndiko vinakoanza kupatikana vipaji.

Dk. Shein aliyasema hayo alipokuwa na mazungumzo na uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Ikulu mjini Zanzibar wakati Wizara hiyo ilipokuwa ikiwasilisha taarifa ya utekelezaji Mpango Kazi wake wa robo ya kwanza na ya pili ya bajeti ya mwaka 2011/2012.


Katika maelezo yake Dk. Shein alisema siku za nyuma michezo ilishamiri kwa kasi na kuwa na vuguvugu na shamrashamra katika skuli hapa nchini hali ambayo ilipelekea kutoa wanamichezo kadhaa wenye vipaji.

Kutokana na hatua hiyo Dk. Shein alisema ipo haja kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuweka mikakati maalum ya kufufua michezo katika skuli kuanzia darasa la kwanza na kuendelea.

Alieleza kuwa michezo ya skuli inasaidia kwa kiasi kikubwa kuwafanya wanafunzi kuwa wakakamavu pamoja na kuwajenga upeo wa ufahamu wa masomo yao.

“Kusoma sio kila wakati mwanafunzi kakamata vitabu tu… ni lazima apate muda apumzike na acheze, kwani michezo pia ni sehemu ya masomo sisi wenyewe enzi zetu tulishiriki michezo tukiwa skuli’, alisisitiza Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein alisema ipo haja kukaa pamoja na kuangalia uwezekano wa kufufua michezo maskulini huku juhudi zikifanyika kuwatafuta walimu wataalamu wa fani hiyo kwani wapo.

Dk. Shein alieleza kuwa sifa zote za Zanzibar katika michezo wakati huo zimeanza katika maskuli hivyo kuna haja hata kuweka vipindi maalum vya michezo darasani na kuimarisha mashindano yenye msisimko kama
ilivyokuwa hapo siku za nyuma.

Akieleza juu ya wazee wanaowakataza watoto wao kutoshiriki michezo maskulini, Dk. Shein alisema kuwa ipo haja kwa Wizara kuwaelimisha wazee hao kutokana na umuhimu uliopo.

Alisema kuwa hatua hiyo ya baadhi ya wazee kutotaka watoto wao kushiriki michezo imekuja kutokana na kutokuwepo kwa elimu ya jamii kwani hapo siku za nyuma hakuna mzee aliyekataa mtoto wake kushiriki
michezo kwani faida yake alikuwa akiiona.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi nia yake ni kuimarisha sekta ya michezo kwani anatambua kuwa ni sehemu ya maisha ya mwanadamu.

Dk. Shein alieleza kuwa kutokana na uamuzi wake huo na kuamini kuwa katika maeneo hayo wanamichezo wa fani zote wanaweza kupatikana juhudi atazichukuwa za kuhakikisha wafadhili wa kuinua sekta hiyo maskulini wanapatikana kwani wapo.

Nao uongozi wa Wizara hiyo ya Elimu na Mafunzo ya Amali ulieleza kuwa juhudi zinachukuliwa na zitaendelea kuchukuliwa katika kuimarisha sekta hiyo maskulini kwani tayari wameshaiweka katika mitaala yao.

2 comments:

  1. Upele kapewa msi kucha!!!!!! Rais kuna mambo mengi tu yanayojitokeza katika kuimarisah elimu kwanini usitumie furasa hii ya kukutana na wizara elimu kujadili mapungufu yaliyopo katika sekta ya elimu na kuyapangia mikakati. Au muandishi uliguswa hii habari ya michezo tuu. Wenzetu ili kukuza vipaji hutumia co-currriculum maskulini michezo ni eneo dogo tuu la kukuza vipaji. Yaonekana tuna sfari ndefu sana kuelekea maendeleo. Huenda ikawa viongozi wetu wana upeo finyu sana katka kudadisi mambo.

    ReplyDelete
  2. Duu!..kaka naunga mkono hoja 'mia -fil-mia'
    Maendeleo ya nchi yeyote duniani hutegemea uimara wa mfumo wake wa elimu na jamii inayochezea elimu,.. kwa keli hua haitoki!

    Wadau wa elimu msichoke, wazindueni jamaa hao wasituulie vipaji vya vijana wetu!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.