Ataka wananchi wawakatae, serikali yachoka nao
Na Mwantanga Ame
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amesema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, itawakataa viongozi wote wanaohusika kuchochea migogoro ya ardhi.
Balozi Seif alisema hayo jana Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar kwenye hotuba yake ya kuuahirisha mkutano wa sita kikao cha nne cha Baraza la Wawakilishi, kilichochukua muda wa wiki mbili.
Alisema serikali itawakataa viongozi wa namna hiyo kwani hawafai katika kuitumikia nchi kwa kuwaongoza wananchi, ambapo kauli hiyo iliwafanya wajumbe wa Baraza hilo kugonga meza kwa kumuunga mkono.
Balozi Seif alifahamisha kuwa kiongozi yoyote anayetumia madaraka yake vibaya kwa kupora ardhi huyo hafai kuongoza serikali kwani ameonesha kuwa ni mlafi, aliejaa tamaa na lazima watu wa aina hiyo wakataliwe.
Alisema inasikitisha kuona masheha, madiwani kuwa ndio vinara wa kutengeneza migogoro ya ardhi katika maeneo yao, kwa kushirikiana na wananchi wakorofi waliojaa tama ya kujipatia fedha.
“Sisi viongozi kwa upande mwengine tunahusika na migogoro hii, masheha, madiwani wanachangia kwa asilimia kubwa katika maeneo ya utalii kiongozi anayeonesha njia inayoelekea kwenye uporaji wa ardhi
hatufai”, alisema Balozi Seif.
Alisema kuongezeka kwa thamani ya ardhi hasa maeneo ya uwekezaji, imesababisha baadhi ya viongozi kujiingiza katika kuchochea migogoro ardhi lakini serikali itawakataa viongozi wa namna hiyo.
Alisema kiongozi bora, ni yule anaetekeleza majukumu yake kwa kuwaonesha njia nzuri kwa anaowatumikia ili awape matumaini wananchi anaowaongoza na sio kuwabughudhi kama ilivyo sasa katika migogoro ya
ardhi inayotokea hapa nchini.
Balozi Seif, alisema hivi sasa mikoa yote ya Unguja na Pemba, imekumbwa na migogoro ya ardhi, ambapo Kusini na Kaskazini Unguja ikiwa inaongoza katika vijiji vya Kiwenga, Pwani mchangani na Nungwi na upande wa Kusini ni kijiji cha Mtende.
Kutokana na hali hiyo, Balozi Seif, alisema ni vyema kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuchukua jukumu la kuwapatia elimu wananchi katika majimbo yao, ili waweze kufahamu na kutafuta usuluhishi huku
wakiwasaidia kuwashauri kuacha tamaa na masheha kuacha tabia ya utapeli.
Akizungumzia zoezi la sensa lijalo Makamu huyo alisema wananchi wasiliogope zoezi hilo litapowadia na jamii ishiriki ipasavyo kwani litaisaidia serikali kupanga mambo yake vyema katika mipango yake ya maendeleo.
Alisema hivi sasa, serikali imo katika utekelezaji wa mpango wake wa kupunguza umasikini MKUZA na Malengo ya Milenia 2015, hivyo zoezi hilo la sensa litasaidia sana kufanikiwa kwa mipango na mikakati hiyo ya kimaendeleo.
Akizungumzia juu ya suala la azma ya serikali katika kuleta mapinduzi ya kilimo, alisema serikali itahakikisha kuwa inatimiza malengo yake kwa kuwapatia ruzuku wakulima wote wa Zanzibar ili pawepo na uhakika
wa chakula.
Alisema hadi kufikia hadi kufikia Januari 2012, Shirika la Biashara la Taifa, limeweza kununua tani 4,479 na kutumia shilingi bilioni 66.95 na ni vyema wakulima wakajenga utamaduni wa kuweka fedha benki.
Akizungumzia sekta ya utalii, alisema imepata mafanikio kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watalii kutoka 132,836 kwa mwaka 2010 na kufikia 175,670 kwa mwaka huu na ni vyema taasisi inayosimamia watalii
ikaongeza jitihada hizo.
Katika hotuba hiyo Balozi Seif aliwasisitiza wananchi kushiriki katika kutoa maoni kwenye mchakato wa uundwaji wa katiba mpya ya Tanzania.
Balozi Seif, alisema hivi sasa serikali imo katika utekelezaji wa makubaliano ya kimataifa katika kudhibiti matumizi ya mfumo wa analogi na kwenda digitali ni vyema wananchi wakaona umuhimu wa kushiriki ili
kuepusha kupata matatizo hapo baadae.
Kuhusu miswada iliyopitishwa na Wajumbe hao Balozi Seif alisema serikali itahakikisha sheria hizo zitapokamilika wanazitumia vyema katika kufanya maamuzi ya serikali huku akiahidi kuwa serikali itaurejesha tena mswada wa mafao ya viongozi katika kikao kijacho cha Baraza hilo.
Balozi Seif, aliatoa hoja barazani humo ya kukiahirisha kikao hicho hadi Machi 28 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment