Ni wa Jimbo la Muyuni
Atoka rumande kwa dhamana
Na Mwantanga Ame
BARAZA la Wawakilishi limethibitisha mjumbe wake kutoka Jimbo la Muyuni, Jaku Hashim Ayoub, kukamatwa na polisi akikabiliwa na shutuma za kuhusika na kuzama kwa meli ya Mv. Spice Islanders.
Akitoa taarifa kwa wajumbe wa Baraza hilo jana baada ya dua mbili za kuliombea Baraza na serikali, Spika Pandu Ameir Kificho alisema mjumbe wake huyo aliyechaguliwa na wananchi wa Muyuni alikamatwa na Polisi na kuhojiwa.
Kwa mujibu wa Spika huyo, Mwakilishi huyo juzi jioni alifikishwa kituo cha Polisi, na kuhojiwa kutokana na kutajwa katika ripoti ya Tume ya kuchunguza ajali ya kuzama kwa meli hiyo iliyoua watu wapatao 203.
Alisema kwa mujibu wa kanuni ya 38 (1), inayotoa kinga, Haki na Fursa za Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, kifungu cha nne ya mwaka 2007, kinaelezea juu ya kuwekewa haki na kinga kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, hivyo anapaswa kuwaeleza wajumbe waelewe hali iliyopo.
Kutokana na hali hiyo Spika Kificho, alisema Januari 18 mwaka huu majira ya saa 11 za jioni alipokea taarifa kutoka kwa Kamishna wa Polisi Zanzibar, juu ya kukamatwa kwa mjumbe huyo ambaye alihojiwa kwa
saa kadhaa na jeshi hilo.
Alisema baada ya kuhojiwa Mwakilishi huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa, ili aweze kujibu tuhuma zake dhidi ya kadhia ya kuzama kwa meli hiyo.
“Nimepokea kwa mshituko kukamatwa kwa mjumbe wangu huyu, Jeshi la Polisi limeniarifu amehojiwa na kuachiwa kwa dhamana kwa hiyo wajumbe wa Baraza naomba mlitambue hili”, alisema Kificho katika taarifa yake.
Baada ya kutoa taarifa hiyo mjumbe huyo pia wakati akitaka kujibiwa suala lake alisema anasikitishwa na hatua ya jeshi la Polisi kumuhusisha katika sakata hilo, kwani yeye hayumo katika umiliki wa meli hiyo.
Alisema kinachoonekana kwa Jeshi hilo la Polisi kuamua kumkamata na kumfikisha Mahakamani kwa dhamira ya kumdhalilisha na kumvunjia heshima na hadhi yake.
Hata hivyo Mwakilishi huyo, aliwataka wananchi wa Jimbo la Muyuni kutulia kusubiri hatma ya suala hilo.
Matamshi hayo Spika wa Baraza la Wawakilishi alimtaka Mwakilishi huyo kutoyatumia ndani ya chombo hicho kwa vile yapo katika misingi ya kisheria.
Wiki iliyopita zaidi ya watu 10 walifikishwa Mahakama Kuu ya mjini Zanzibar, wakikabiliwa na tuhuma za kuhusika na uzembe uliosababisha kuzama kwa meli ya Mv. Spice Islanders Septemba 10 mwaka jana huko
Nungwi mkoa wa Kaskazini Unguja.
No comments:
Post a Comment