Habari za Punde

Aanguka na Kujifungua nje ya Wodi

Ni baada ya wauguzi kukataa kumsaidia

Khamisuu Abdallah na Madina Issa

MAMA mmoja anaetambulika kwa jina la Mwantatu Kombo mkaazi wa Miembeni ameelezea kusikitishwa kwake kwa kitendo alichofanyiwa na wauguzi wa hospitali ya Mnazimoja wodi ya wazazi wakati alipokwenda kumpeleka jamaa yake kwa ajili ya kujifungua.

Akisimulia mkasa huo Mwantatu alisema kuwa tukio hilo lilitokea wiki iliyopita majira ya saa 9 usiku, ambapo alifika hospitalini hapo kwa lengo la kumpeleka jamaa yake na hatimaye kujifungua nje ya wodi ya wazazi hospitalini hapo.

Alisema alipofika wodini hapo akiwa amefuatana na mjamzito huyo, anaejulikana kwa jina la Fatma Ali Suleiman ambaye alimuomba ampatie msaada wa kumpeleka hospitali, lakini hakupokelewa kutoka na kutokuwa na vifaa.


Alisema kutokana na kutokuwa na vifaa, aliambiwa na wauguzi hao atoke nje na hawatompokea mjamzito huyo pamoja na kuwaeleza kuwa atavilipia baada ya kujifungua kutokana na hali yake.

Pamoja na Mwantatu kudai kuwafahamisha yote hayo kuhusu mzazi wake lakini madaktari hao hawakumsikiliza kilio chake na kumtaka atoke nje yeye na mjamzito wake huku mzazi huyo akiwa na uchugu na tayari kwa kujifungua.

"Wakati nikiwa natoka nje na mjamzito wangu, alianguka mbele ya wodi ya wazazi na kujifungua hapo hapo chini, mara baada ya kujifungua nilirudi kwa wauguzi kuwambia mgonjwa wangu ameshajifungua nje naomba kuomba msaada lakini pia walikataa.

Kwa upande wake Mzazi huyo Fatma Ali alisema kuwa mwanzo wa kupata ujauzito huo alikwenda kupima na kuambiwa atoe shilingi 10,000 kwa ajili ya kununua gamba na hali yake alikuwa hana hata shilingi na ndipo akaondoka na kwenda zake hadi kujifungua kwake.

Kwa upande wake Msaidizi Katibu hospitali ya Mnazimmoja Mohammed Nadi alithibitisha kutokea tukio hilo kwa madaktari hao na alisema kitendo walichokifanya wauguzi kwa kumuacha mzazi kujifungua nje ya wodi si kitendo cha kiungwana.


Akizungumzia kadhia hiyo Katibu wa Hospitali ya Mnazimmoja, Omar Abdalla Ali, aliwashauri wananchi wanapofanyiwa vitendo vya udhalilishaji wawe na utaratibu wa kuripoti kwa ushahidi wa kutosha pamoja na kufika katika vyombo vya sheria kwa ajili ya hatua za kisheria zaidi.

"Mara baada ya tukio hilo tuliwaandikia barua na kutaka wajieleze lakini hatukuridhika na maelezo yao waliyoyathibitisha kwenye barua yao, hivyo nitawaita kwenye kamati ya maadili wiki ijayo kwa ajili ya kusikiliza pande zote mbili na kulichukulia hatua za kisheria zinazofaa”, alisema Msaidizi huyo.

Aidha aliwataka madaktari kuachana na vitendo vya rushwa ambapo hivi sasa vimeonekana kukithiri kwa kiasi kikubwa na kupelekea kutothamini utu na binadamu.

Barua yenye ripoti kutoka kwa Muuguzi wa Maternity Ward ya Februari 2 mwaka huu, imeeleza kwamba siku ya tarehe saba mwezi huu wauguzi wawili (majina tunayahifadhi) walimpokea mgonjwa vizuri na wamemuweka katika kochi na kabla hawajamchunguza walimtaka atowe vifaa vyake, jamaa zake walijibu hawana na walielekezwa wakanunue hospitali ya Al-Rahma.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa walidai hawana pesa, wakati wanamuelekeza mgonjwa akalale kwenye kitanda, wauguzi hao waliitwa kwenda kumhudumia mgonjwa mwengine mwenye Eclampisia.

Ilieleza taarifa hiyo kuwa walipokuwa wakimshughulikia mgonjwa wa Eclampisia, mama wa jamaa zake walitoka nje na baadae wauguzi walipata taarifa ya mama ameshajifungua walipoulizwa wakunga aliemsaidia mama huyu ni nani, walijibu hawamjui maana wao hawakwenda tena, ilimaliza ripoti hiyo.

6 comments:

  1. Subhana-Allah! Hivi jamani huo utu uko wapi hapa? Binadam hata hawajali roho ya binadam mwenzao? Haya ni maisha ya mtu hivi roho imekuwa haina thamani nyumbani kwetu hadi kufikia hali hii? Inasikitisha sana sijui serikali yetu iko wapi pamoja na wakuu wake wakalielezea suali hili? Ni aibu na ni unyama wa mwisho. Sasa kwa hao maskini za Mungu wasio na kitu waende wapi na hapo Mnazi mmoja ndiyo pa serikali ambayo ni ya wananchi wote zaidi wasiyo na uwezo! Mola atuvushe na hayo na awape imani watu wetu angalau wajali na kuthamini roho ya binadam, amiin.

    ReplyDelete
  2. Ni kisa cha kutoa machozi kwa kuona sisi Waislamu wa Kizanzibari tumeshafikia hali hiyo ninayoweza kuiita ya kinyama. Serikali ina makosa yake lakini na Wauguzi wana makosa yao. Sababu waliyoitoa inaonyesha ni ya kupanga kuogopa kuadhibiwa. Wanasiasa wanafikiria kujiongezea posho tuu kwa jasho la wananchi bila kuwajali hao wanaowalipa hizo posho zao. Ama kweli mnyonge myongeni. Jee tutafika.

    ReplyDelete
  3. inasikitisha sana.panahitajika mengi ya kujiuliza ,vipi yametokea ,nani wa kulaumiwa ,na khatua gani za kuchukuliwa isije kujiri kutokea tena mambo km haya,
    mungu atupe imani na uwezo wa kuyakabil mas ala km haya,ameen

    ReplyDelete
  4. asalamu alaykum.
    Mr Mapara hii kesi pls itolewe kwenye magazeti na mawio yenu ili watu wajue uzembe wa kweli kwa wauguzi wetu hasa wakunga.napia ifuatilie ili tujuwe ni hatua gani zimechukuliwa kwa wauwaji hawa ni wauwaji kabisa tena si binadamu hawa.

    ReplyDelete
  5. Juma Duni hao waliokuwa zamu usiku huo wafunguliwe mashtaka na kwa kuanzia wawe suspended. Haya ni mauaji. Sisi tunapiga vita kuikomboa nchi yetu kumbe kuna watu wanasaidia maovu ndani ya sisi wenyewe.

    ReplyDelete
  6. ni kweli kisa cha kusikitisha sana kwamba utu na ubinaadamu wetu unaondoka, na wahusika wanatakiwa wachukuliwe hatua za kinidhamu baada ya uchunguzi wa kutosha.lakini tunatakiwa tuangalie masuala km haya katika nyanja nyingi what are the source of this? limetokea kwa sababu nyingi,za kiuchumi na kijamii na kisiasa pia.
    1)kiuchumi- kitu gani kinachopelekea hospitali ikaekewa budget ndogo mpk ikapelekea kukosekana essential kits ambapo kwa siku vinahitajika vifaa vya kujifungulia zaidi ya 50 inategemea na.number ya wazazi. viongozi wetu wakuwapi? wanapigia debe kuengezea allowancesna sio budget za social services na kuwa na good leadership.
    1)wkisiasa- ni nini hasa sababu ya kukimbia wataalamu wetu kwetu zanzibar, tunatumia gharama kubwa kuwasomesha then hakuna anaeonekana, watu wanafuatilia maslahi kwengine kwa vile kazi zao ni ngumu na hakuna maslahi yanayoboreshwa zikiwemo, call allowances, risk allowances ziko wapi.kuweko kwa nurse 1 au 2 katika wodi hasa usiku kwa kumunitor na kuzaisha wamama si chini ya 30 kwa usiku na kila mmoja anacomplication zake na kesi zinatafautiana, matatizo km haya yatachukua muda kupungua. tunahitaji kuengeza nguvu kazi( human resources) na kuwa na uzalendo na upendo wa kazi zetu ili kupunguza matatizo ya kijamii.
    3) Mbali ya kufata elimu ya Afya, kituo cha afya, jamii nayo hasa akina mama ndo wahanga wakuu tunatakiwa tuelimishane umuhimu wa kujitayarisha na mahitaji muhimu ikiwemo vifaa wakati tukiwa wajawazito, Tuchukulie kesi kama inatokea nyumbani hakuwahi kufika hospitali ingekuwaje?Akina baba tunatakiwa tuchukue majukumu yetu,kwa mujibu wa uwezo wetu, tuzingatie mambo muhimu wakati mama anapokuwa njamzito, na nafkiri jamii yetu yakizanzibar ipo tayari kusaidia masuala kama haya, mtu unapoeleza ukweli shida yako.kwa pamoja tunaweza naomba , tushirikiane kwa pamoja, tuelimishane, tusaidiane majukumu ili tuweze kutatua matatizo ya kijamii

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.