Habari za Punde

Bidhaa Chakavu Kupandishwa Ushuru

Lengo kudhibiti uharibifu mazingira

Na Mwantanga Ame

WIZARA ya Nchi ofisi ya Rais Fedha, Uchumi Mipango na Maendeleo inajiandaa kupandisha ushuru kwa vifaa vichakavu ili kudhibiti uingiaji vifaa hivyo nchini.

Waziri wa wizara hiyo Omar Yussuf Mzee, aliyasema hayo alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Waziri Omar, alisema serikali inalazimika kuchukua hatua hiyo ya kupandisha ushuru wa vifaa hivyo ili kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na vifaa hivyo ambavyo vimekuwa vikiingizwa kwa wingi.


Alisema vifaa hivyo kuachwa kuingia nchini ipo hatari kubwa ya serikali kujikuta kushindwa kuviangamiza kutokana na vingi haviwezi kutumika kutokana na kupitwa na mfumo wa teknolojia ya kisasa ya digitali.

Alisema hatua hiyo inayotaka kuchukuliwa ya kuongeza ushuru imekuja kutokana na mwezi Disemba mwaka huu, kuwa muda wa mwisho unaozitaka nchi zote za Afrika Mashariki kuingia katika mfumo wa dijitali na kutoka katika mfumo wa analogi.

Kutokana na hali hiyo, waziri huyo alisema, Zanzibar inapaswa kujiandaa kwa kuwa na mkakati madhubuti utaoweza kudhibiti vifaa aina ya analogi kutoingizwa nchini.

Alisema hivi sasa kumekuwa na kiwango kikubwa cha vifaa chakavu vinavyoingizwa nchini jambo ambalo huenda likasababisha hatari wakati zoezi hilo litapoanza kutumika.

Alisema vingi ya vifaa vinavyoingizwa hivi sasa viko katika mfumo wa analogi, ambao tayari ifikapo muda huo havitaweza kutumika, jambo ambalo litawasababishia hasara wananchi.

Waziri huyo alisema katika kudhibiti hali hiyo isitokee Wizara hiyo inakusudia katika bajeti yake ijayo kwenda na pendekezo la kupandisha ushuru kwa vifaa chakavu kuwa mkubwa hatua itayowafanya waingizaji wa vifaa hivyo kutoleta nchini.

Aidha, Waziri huyo alisema vifaa hivyo hivi sasa tayari vimebainika vinapoingizwa nchini vikiwa na mende ambao ni hatari kwa afya ya jamii huku vikiwa na kemikali za sumu ambazo zinaweza kuleta athari za kimazingira hapo baadae.

Mrajis wa Tume ya Utangazaji Zanzibar, Abdalla Mitawi, akizungumzia juu ya hatari inayoweza kutokea alisema itamgusa kila mwananchi na serikali inaweza kupata lawama kwa kushindwa kuwatimizia haki ya kikatiba ya kupata matangazo wananchi.

Alisema kutokana na hali hiyo serikali italazimika kuhakikisha inabadili mfumo wa mawasiliano kutoka analogi kwenda digitali huku wakikabiliwa na tatizo la kuziangamiza televisheni zilizotengenezwa kwa mfumo wa analogi.

Alisema zoezi la mabadiliko hayo serikali ya Zanzibar itahitaji kutumia dola za kimarekani bilioni 28.5 ambapo tayari serikali imefanya mazungumzo na Benki ya EXIM ya nchini China kuweza kupata mkopo huo.

1 comment:

  1. Haya, ni mamabo ya kuiga na yatatutia umaskini!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.