MTU mmoja mkaazi wa Micheweni Mjini, Sharif Omar Ali (40) amefariki dunia baada ya kuangukiwa na jiwe alipokuwa akichimba mawe eneo la Mkwajumgoro Micheweni Pemba.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Yahya Rashid Bugi, alisema mtu huyo alifariki dunia wakati akikimbizwa katika hospitali ya Micheweni majira ya saa 5.30 mchana baada ya kuangukiwa na jiwe hilo.
Alisema kuwa wananchi wanapokuwa katika kazi ya uchimbaji wa mawe wawe na tahadhari kwani kazi hiyo imekuwa ikipoteza maisha ya watu kila mwaka.
Aliwataka wananachi wa Micheweni na vitongoji vyake kutokuingia katika mivungu ya mawe wakati wa uchimbaji kutokana na uwezekano wa mawe hayo kukatika na kumuangukia aliyekuwemo shimoni.
Nao mashuhuda ambao walikuwa pamoja na marehemu huyo, Shaame Shoka Haji (34) alisema kuwa walikuwa jirani wakati wakichimba mawe na baada ya muda waliona jiwe kubwa limeanguka na kumuangukia marehemu huyo.
“Sisi tulikuwa pamoja katika kazi hiyo lakini kila mmoja alikuwa mahala pake na tuliona jiwe limemuangukia mwenzetu na sisi tukapiga kelele kuomba msaada, kwani jiwe lilikuwa kubwa sana”, alisema shuhuda huyo.
Nae shuhuda mwengine, Mussa Ali Ayoub, (30) mkaazi wa Micheweni, alisema kuwa walifanya juhudi ya kumuokoa marehemu, lakini walishindwa kutokana na ukubwa wa jiwe lililomlalia.
“Baada ya kulikata jiwe ndipo tukampata na tukamkimbiza hospitali ya Micheweni Pemba, akiwa mzima, lakini tukiwa njiani alifariki”, alieleza.
Daktari dhamana wa hospitali ya Micheweni, Khamis Rashid Mohammed, akiwa na muuguzi mkuu hospitali hiyo, Mohammed Ali Salim, walieleza kuwa marehemu alipoteza damu nyingi wakati wa ajali hiyo, kwani alipata majeraha ya ndani na kuumia kwa kichwa na mguu.
Akizungunza na wananchi Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Utamaduni, Utalii na Michezo, Bihindi Hamad Khamis na Mbunge wa Mimbo la Micheweni, Haji Khatib Kai, baada ya tukio hilo aliwataka wananchi kufuata taaluma ya uchimbaji mawe na kokoto kwani ni faida kwao na inasaidia katika kuondoa ajali kama hizo.
Hivyo waliwataka wafiwa kuwa na subra wakati huu na kwamba kila mmoja mauti yatamfika kwa pale alipo andikiwa.
No comments:
Post a Comment