Habari za Punde

Cannavaro Kuikimbia Taifa Stars

Na Salum Vuai, Maelezo

SIKU chache baada ya Kocha Mkuu wa Taifa Stars Jan Poulsen kutangaza kikosi kitakachoivaa timu ya Taifa ya Msumbiji, beki mahiri aliyeachwa Nadir Haroub 'Cannavaro', amesema yuko njia kujiuzulu kuichezea timu hiyo.

Stars imepangwa kupambana na timu ya Taifa ya Msumbiji wiki ijayo, katika mchezo wa kusaka tiketi ya mashindano ya mataifa ya Afrika mwaka 2014 yanayotarajiwa kufanyika nchini Afrika Kusini.


Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, beki huyo wa mabingwa wa soka Tanzania Bara Yanga na Zanzibar Heroes, amesema uamuzi huo hautokani na kutemwa katika kikosi hicho, bali ameona
wakati umefika kuwaachia vijana wengine kutoa mchango wao.

Cannavaro ambaye ni nahodha msaidizi wa Stars, hayumo kwenye kikosi kilichotajwa na Poulsen hivi karibuni, ambacho kinajiandaa na mechi hiyo iliyopangwa kuchezwa Februari 29 katika uwanja wa Taifa jijini
Dar es Salaam.

Nyota huyo mwenye sifa ya kucheza jihadi sehemu ya ulinzi wa kati, amesema anakusudia kuelekeza nguvu zaidi katika kuitumikia klabu yake ya Yanga, inayopigana kutetea ubingwa wa Bara ilioutwaa msimu uliopita.

Alipoulizwa iwapo ana nia ya kujiuzulu kuichezea timu ya Taifa ya Zanzibar, 'The Zanzibar Heroes' pia, Cannavaro alisema hafikirii kuacha timu hiyo na ataendelea kuitumikia kwa moyo wake wote hadi
makocha watakapoona uwezo wake umekwisha.

Beki huyo amekuwa chaguo la kwanza tangu Taifa Stars ilipoanza kufundishwa na Marcio Maximo kutoka Brazil, na kurithiwa na Poulsen, akijijengea jina kutokana na staili yake ya ukabaji.

Mwaka juzi, Cannavaro aligonga vichwa vya habari kwa kitendo chake cha kubadilishana jezi na mchezaji Samuel Eto'o wa Cameroon baada ya mchezo kati ya Stars na timu hiyo, ambacho kiliibua hisia tafauti
kutika kwa wapenzi na wadau wa soka nchini, baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kumtaka alipie jezi hiyo.

Taifa Stars inatarajiwa kupambana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kesho kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, katika mchezo wa kirafiki kabla kuivaa Msumbiji Februari 29 mwaka huu.

3 comments:

  1. bora mwana maana dharau zimezidi kwa wazanzibar tuko pamoja na wewe kaka Canavaro

    ReplyDelete
  2. Bora achana na timu ya Taifa ya Tanganyika wabaguzi tu hao....

    ReplyDelete
  3. safi sana mwanangu nimependa uliposema utaitumikia Zanzibar Heroes kwa moyo wako wote tuko pamoja na zidisha bidii tutafika tu ishaallah

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.