Habari za Punde

Mfumo Dume Wachochea Udhalilishaji Kaskazini Unguja

Na Madina Issa

MKUU wa wilaya ya Kaskazini ‘A’ Riziki Juma Simai, amesema kati ya mambo yanayosababisha kuongezeka kwa vitendo vya udhalilishaji katika mkoa huo ni kushamiri kwa mfumo dume kwenye familia.

Aliyasema hayo alipofungua kongamano la majadiliano ya usawa wa kijinsia na kupinga vita dhidi ya udhalilishaji kwa wanawake, watoto na vijana wa mkoa wa kaskazini Unguja uliofanyika kituo cha Mafunzo ya Amali Mkokotoni.

Alisema kuongezeka kwa mfumo huo kunachangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa udhalilishaji katika jamii.


Aidha alisema hivi sasa mkoa wake unaendelea kuandaa mipango madhubuti ili kuweza kupunguza vitendo vya ukatili kwa watoto wa jinsia tofauti.

Hata hivyo aliwasihi wanamafunzo hao kuyafanyia kazi na kutoa michango itakayofanikisha kupunguza au kuondosha kabisa vitendo vya udhalilishaji, unyanyasaji na ubaguzi wa kijinsia ili jamii iweze kufaidika na kupunguza vitendo vya ukatili katika Mkoa wa Kaskazini.

Nae Afisa msaidizi wa elimu Mkoa wa Kaskazini, Maulid Nafasi alisema unyanyasaji, udhalilishaji na ubaguzi wa kijinsia ni janga la kutisha katika jamii ya wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Hata hivyo alifahamisha kuwa kinachijitokeza hivi sasa ni tabia ya malezi kwa watoto na wazazi sio ya pamoja ambapo ndio sababu inayowafanya kushamiri kwa vitendo vya udhalilishaji.

Afisa huyo alisema katika mkoa wake hivi sasa wameandaa mikakati ya kupita kila shehia na kuwaelimisha wananchi juu ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kwa watoto.

Pia alisema pamoja na kuhakikisha kila shehia inanzisha kamati endelevu inayohusiana na vitendo hivyo pamoja na kufuatilia utekelezaji wa kamati za shehia.

Mmoja wa wanamafunzo hao Mwajuma Kassim, akichangia kongamano hilo alisema urasimu unakuwa mkubwa katika kusikiliza kesi za udhalilishaji ndio maana hazipungui katika mkoa huo.

Hivyo alilitaka jeshi la Polisi mkoani humo, watakapowabaini watu wanaowafanyia vitendo vya ukatili watoto, wasipewe dhamana kwani dhamana hizo ndio inayopelekea kuongezeka kwa vitendo hivyo.

Mafunzo hayo ya siku moja yameandaliwa na mtandao wa asasi za kiraia wa Mkoa wa Kaskazini na kudhaminiwa na Foundation for Civil Society.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.