Habari za Punde

Nyumba Nane Zateketea kwa Moto

Na Mwantanga Ame

CHUNGU cha mboga alichoachiwa mtoto wa miaka saba kimeteketeza nyumba nane katika kijiji cha Mchekeni Wilaya Kaskazini ‘B’ Unguja.

Tukio hilo limetokea juzi jioni majira ya saa 10.00 jioni wakati mtoto huyo alipoachiwa upishi huo mama yake akiwa amekwenda kondeni.


Moto huo umesababisha zaidi ya watu 30 kukosa makaazi huku mali za mamilioni ya fedha zikiwa zimeteketea zikiwemo nyumba nane na fedha taslimu za baadhi ya wakaazi hao.

Wakisimulia tukio hilo baadhi ya majirani walioathirika na moto huo walieleza kuwa Mama wa mtoto huyo waliemtaja kwa jina la Maryamu na mume wake Sixty, waliondoka na kumkabidhi binti yao Rehema huku
wakiwaomba wamsimamie afanikishe chungu cha mboga alichoachiwa.

Walisema baada ya muda walimkuta mtoto huyo akicheza na wenzake na kumtaka aende kukiangalia chungu cha mboga kinavyondelea upishi wake lakini alikuta kikiwa moto umezimika.

Walisema baada ya mtoto huyo kuona hali hiyo aliamua kuwasha tena moto na kutoka nje lakini aliporudi alikuta moto ukiwa umepamba katika paa lao huku kukiwa na moshi mzito.

Baada ya kuiona hali hiyo mashuhuda hao walieleza mtoto huyo alitoka na kwenda kuwaarifu majirani zake lakini walipokwenda walikuta moto huo tayari umeshika na nyumba nyengine.

Alisema baada ya kuiona hali hiyo wananchi hao walisema walijaribu kuuzima moto huo lakini kutokana na upepo ulizidi kupamba moto.

Hata hivyo wananchi hao walieleza kuwa kazi waliyoifanya baada ya kuona hali inazidi kuwa ngumu waliamua kuokoa mali zao lakini baadhi ya vitu vilishindwa kuokolewa kutokana na moto huo kuwa mkubwa.

Wananchi hao walieleza ndipo walipoamua kuwasiliana na kituo cha Zima moto Cha Wilaya ya Kaskazini ‘B’ ambao walikwenda na kufanikiwa kuuzima moto huo.

Akizungumza na waathirika hao, Mke wa Makamu wa Pili wa Rais Mama Asha Seif Iddi, aliwapa pole kwa tukio hilo na kuahidi kuwapatia msaada.

Mama Asha alijitolea kuwapatika makaazi ya muda katika Tawi la Jimbo la Kitope, pamoja na kuwakabidhi fedha kwa ajili ya kujikimu huku wakifikiria njia nyengine za kuwasaidia ili warudi katika makaazi yao.

Wananchi hao walimshukuru mama Asha na kuahidi kushirikiana nae huku wakiangalia hasara iliyowapata na kutafuta njia za kutatua tatizo hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.