Habari za Punde

Wafungwa Zanzibar Kuvaa Kama Ulaya

Na Mwantanga Ame

BAADA ya kilio kikubwa cha wanaharakati na makundi ya kutetea haki za binadamu juu ya kuyapinga mavazi ya wanafunzi wa Vyuo vya Mafunzo Zanzibar, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inajiandaa kubadili mavazi hayo kwa kuwapatia nguo mpya wanafunzi hao.

Wanaharakati na viongozi wa kisiasa Zanzibar, mara kadhaa walitoa kauli za kuyapinga mavazi ya wanafunzi hao kwa kudai yalikuwa yakiwadhalilisha ndani ya jamii.

Madai ya Wanaharakati hayo yalieleza kuwa mavazi hayo ya kuvalishwa suruali za kaptula na shati haziendani na maadili ya utu wa kibinadamu kutokana na baadhi ya wanafunzi wanaingizwa katika vyuo hivyo wakiwa ni watu wazima na wenye familia.


Wanaharakati hao walidai hadhi hiyo ya wanafunzi inakuwa mbaya zaidi katika kupoteza utu wake pale wanapotolewa kufanya kazi katika maeneo ya kijamii ambapo huweza kukutana na familia yake akiwa katika mavazi yasioridhisha wakati akiwa huru.

Kutokana na hali hiyo serikali ya Zanzibar imesema kuwa wakati wowote kuanzia sasa inabadili mavazi hayo kwa kuwapatia nguo mpya ambazo zitaweza kurudisha utu wa mwanafunzi hata kama yupo chuoni.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyihaji Makame aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa Habari ikiwa ni utaratibu wa Mawaziri wa Serikali kuelezea majukumu yao katika utekelezaji wa shughuli za serikali.

Alisema mavazi wanayokusudia kuyatoa yatakuwa katika muundo wa suruali ndefu na mashati yatayokuwa katika rangi ya orange badala ya sasa ya bafta ya rangi nyeupe.

Alisema serikali imezingatia kubadili mavazi hayo ikiwa ni kufuata mfumo wa kimataifa ambapo hutaka wanafunzi wa vyuo vya mafunzo kuvaa aina hiyo ya nguo.

Alisema nguo hizo tayari hivi sasa zipo katika hatua za mwisho kukamilika ushonaji wake na wakati wowote serikali itazizindua na kuanza kutumika kwa wanafunzi hao.

Alisema nguo hizo wanatarajia kuwapatia kila mwanafunzi nguo mbili ikiwa ni hatua itayowawezesha kubadili katika mazingira ya maisha yao.

Mbali ya kuimarisha hilo pia Waziri huyo alisema Wizara hiyo hivi sasa imeweza kusimamia vyema kuweka mabadiliko ndani ya vyuo vya Mafunzo kwa kuimarisha maeneo tofauti baada ya kuombwa kufanya hivyo na Tume ya Haki za binadamu.

Akitoa ufafanuzi zaidi Kamishna wa Vyuo Vya Mafunzo Zanzibar, Khalifa Hassan Chum, alisema wamo katika kutekeleza mpango mkubwa wa kukabiliana na msongamano wa wanafunzi katika vyuo hivyo.

Alisema mpango wanaoutekeleza ni unaohusu ujenzi wa jengo jipya la wanafunzi wa Vyuo vya mafunzo ambapo litakuwa lenye mfumo wa kisasa.

Aidha, alifahamisha kuwa wakati wakijenga gereza hilo pia katika mkakati huo wanakusudia kuyafanyia matengenezo jengo la ubago na jengo la kiinua miguu

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.