Na Mwantanga Ame
MKE wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mama Asha Seif Iddi, ameishauri jamii kuwa na utamaduni wa kuwaangalia walimu wa madrasa kwa kutoa fedha za gharama ya masomo wanazotozwa kwa ajili ya masomo yao.
Mama Asha, aliyasema hayo wakati akitoa nasaha zake katika sherehe ya mauled ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad S.A.W, yaliofanyika katika madrasa ya Taalim Islamia ya kijiji cha Kazole Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja.
Alisema ni mambo ya kusikitisha jamii hivi sasa imeacha utamaduni wa kulipia ada inayotozwa na walimu wa madrasa jambo ambalo limekuwa likiwapa ugumu kufanya kazi zao vizuri.
Alisema jambo la kushangaza wakati hali hiyo ikiwepo kwa walimu wa madrasa lakini jamii inakuwa tayari kuwalipia gharama kubwa za maskuli zikiwemo za masomo ya ziada ‘tuition’.
Alisema hali hiyo imekuwa ikiwatia unyonge walimu wa vyuo vya madrasa kiasi ambacho humlazimu kumega muda wa kushughulikia maisha yake jambo ambalo linaweza kukosekana kwa taaluma ya dini ikawa inatolewa kwa kiasi kidogo.
Mama Asha alisema kutokana na hali hiyo ni vyema jamii ikaiona athari inayoweza kutokea ikiwa wataendelea kutolipa ada za masomo kwa ajili ya watoto wao wanaosoma katika vyuo vya Madrasa.
Aidha Mama Asha aliwataka wananchi wanaotumia kusomesha watoto wao kujenga ushirikiano katika kuiendeleza madrasa hiyo kwa vile bado inahitaji kuimarishwa.
Alisema ili mtoto aweze kusoma vizuri anahitaji kuwa na eneo bora la kupata elimu na wasiridhike na hali ya madrasa hiyo ilivyo sasa.
Mama Asha alisema yeye binafsi kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo hilo Balozi Seif Ali Iddi, atakuwa tayari kutoa msaada wa kuiimarisha madrasa hiyo.

Hakuna mzazi anaekataa kulipa ada ya mtoto wake kwa ajili ya madrassa isipokua mfumo wa ufundaji hauridhishi.
ReplyDeleteTakriban miaka 50 sasa tokea tupate uhuru serikali kupitia idara yake ya wakfu na mali ya amana imeshindwa kusimamia mfumko wa elimu ya madrassa.
Leo ktk kila wanafunzi 100 wa madrassa ni takriban watoto 20 tu wanaohitimu, na hao hawana utambulisho wowote( cheti)
Yaani ni kienyeji, kienyeji kienyeji..sasa nani atalipa pesa? kwa mtoto wake kuishia 'lami ya kkun' baada ya miaka mitatu?
Inabidi tubadilike!!!