Habari za Punde

Aliyemdhalilisha mfanyakazi wa hoteli asimamishwa kazi

Na Mwandishi wetu

UONGOZI wa hoteli ya nyota tano ‘5 Stars’ ya RESIDENCE umemsimamisha kazi bosi wa ulinzi katika hoteli hiyo anayedaiwa kutekeleza kitendo cha udhalilishaji cha kumvua nguo za ndani mfanyakazi wa bustani wa hoteli hiyo.

Meneja Mkuu wa hoteli hiyo Yves Montel, alisema menejimenti ya hoteli imesikitishwa na tukio hilo la mfanyakazi wa kike kudhalilishwa ambapo imeona ichukue hatua za kumsimamisha kazi mhusika wa tukio hilo.

Montel alisema tukio hilo la kusikitisha halina ridhaa ya uongozi wa hoteli hiyo na kwamba ni kinyume na maelekezo na maadili ya kazi.

Hatua ya uongozi wa hoteli hiyo iliyopo kijiji cha Mchangamle Mkoa wa Kusini Unguja, imekuja siku moja baada ya gazeti hili kuripoti kadhia nzima ya mfanyakazi wa hoteli hiyo kudhalilishwa, tukio ambalo limeibuliwa na Chama cha Waandishi wa Habari wanawake Tanzania (TAMWA).

Hatutaki kutoa kisingizio chochote, Kitendo kilichotokea kwa mwanamke huyo hakiwezi kukubalika na hatuna mkono wetu katika tukio hilo”, alisema.

“Mlinzi huyo ameshawajibishwa. Lakini tutafanya uchunguzi kamili juu ya tukio hilo ili lisitokee tena,” alisema Yves Montel ambaye alifahamisha kuwa yeye mwenyewe amelifuatilia suala hilo kwa ukamilifu.

Tukio hilo zima lilihusu madai ya mwanamke huyo kwamba ameiba nguo za ndani za mgeni mmoja na ingawa yeye hakuwa na kazi za kwenye vyumba, lakini palikuwa na shaka kwamba nguo hizo zilionekana kwenye kabati lake.

Baada ya uchunguzi mdogo mlinzi huyo mbele za watu alimtaka mwanamke huyo kuvua nguo ili aone alichokivaa ndani au iwapo ameficha nguo zinazodaiwa kuibiwa.

“Kwa maadili yoyote mlinzi yule ambaye ni wa kiume hakutakiwa kumpekua mwanamke huyo kiasi alichofanya”, na kudokeza kuwa kuanzia sasa watasisitiza misingi madhubuti ya kazi kulinda heshima na utu wa watu katika mazingira ya kazi.

Wakati huo huo hoteli hiyo ya Residency itasherehekea mwaka mmoja tokea kuanza kwake ifikapo Machi 30 mwaka huu.

Hoteli ya Residency hapa Zanzibar ni sehemu ya mtandao wa kampuni ambayo iko Thailand, Ufaransa na Tunisia.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.