Habari za Punde

PBC Yalilia Shufaa ya Rais

Na Haji Nassor, Pemba

RAIS wa klabu inayokuza vipaji vya watoto katika mchezo wa mpira wa kikapu kisiwani Pemba (PBC) Hussein Matora, ameiomba Serikali ya Zanzibar kuifadhili klabu hiyo ili iweze kupiga hatua.

Matora alitumia fursa ya mahojiano na Zanzibar Leo, kumuomba Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, kuiangalia klabu hiyo kwa jicho la huruma ikizingatiwa kuwa kiongozi huyo ni mpenzi mkubwa wa watoto na michezo.

Amesema kutokana na sifa hizo za Rais Dk. Shein, iko haja sasa aiongezee nguvu klabu hiyo ya watoto ambayo ni pekee ya aina yake kwa Zanzibar inayojihusisha kikamilifu kuinua vioaji vya vijana katika mchezo huo.


Rais huyo wa PBC alikuwa akizungumza na gazeti hili katika uwanja wa tenisi Chake Chake, wakati wa hafla ya uzinduzi wa klabu hiyo kisiwani humo.

“Kwa kuwa kuimarisha michezo ni miongoni mwa azma za serikali, ni vyema klabu yetu ipatiwe ufadhili ili kuiendeleza dhamira hiyo kwa maslahi ya taifa”, alishauri Matora.

Alieleza kuwa, kwa sasa hawajawa na uwezo wa kuwaweka watoto kwenye jengo maalumu na kuwapa mafunzo ya mchezo huo kutokana na ukosefu wa fedha.

Badala yake, amesema wamekuwa wakihudhuria klabuni hapo kupata mafunzo na baadae kurejea majumbani, jambo ambalo ni zito baadhi ya wakati.

“Kwa hili tunamuomba Mheshimiwa Rais wa Zanzibar atie mkono wake ili tupate ufadhili wa haraka, kwani tuna rasilimali nzuri ya mchezo wa mpira wa kikapu”, alieleza Rais huyo wa PBC.

Akizungumza katika hafla hiyo, Ofisa Mipango Wilaya ya Chake Chake Kassim Ali Omar, alisema hatua ya kuwakusanya watoto hao na kuwapa mafunzo ya mchezo huo ndio pahala pekee pa kuanzia.

Alisema kwa vile mpira wa kikapu haujapewa msukumo wa kutosha, ni vyema mamlaka zinazosimamia michezo nchini, ziitupie macho klabu hiyo ili kuwafungulia vijana milango ya ajira kupitia sekta ya michezo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.