Na Ramadhan Makame
SHIRIKA la Utangazaji Zanzibar (ZBC), linakabiliwa na changamoto ya ushindani katika kukidhi mahitaji ya kihabari kwa wananchi, huku pia kukiwa na sababu kadhaa zinazozorotesha kazi za shirika hilo ikiwemo wafanyakazi kuvunjika moyo.
Samwilu Mwaffisi alieleza hayo alipokuwa akiwasilisha muhtasari wa utafiti uliopangaza utangazaji wa umma Zanzibar katika zama za utangazaji wa ushindani.
Mwaffisi alisema utafiti alioufanya umegundua wafanyakazi wengi wa shirika hilo wamevunjika moyo kutokana, hali inayolifanya shirika hilo kushindwa kuingia katika ushindani na kukidhi mahitaji ya wananchi katika kupata habari.
‘Wafanyakazi wengi wa ZBC wamevunjika moyo kutokana na kukosekana kwa motisha ikiwemo mazingira mazuri ya utendaji kazi’, ilieleza sehemu ya utafiti huyo wa Mwaffisi.
Alisema wafanyakazi waliohojiwa kwenye utafiti huo walieleza vikwazo vilivyopo ni pamoja na kutokuwa na vitendeakazi vya kutosha, huku vile vile vilivyopo pia vikiwa si vya kisasa, kukosekana kwa usafiri, mishahara duni, bajeti finyu na majengo ya kizamani yenye samani chakavu.
Aidha alisema lipo kundi jengine lililofikiwa na utafiti huo, lilieleza kuwa linaridhishwa na utendaji kazi wa ZBC, kutokana na kutoa habari zenye kuaminika zinazotolewa na shirika hilo ikilinganishwa na vyombo vyengine visivyokuwa vya umma.
Pamoja na hali hiyo, utafiti pia umegundua kuwa Wazanzibari wengi ambao ni asilimia 42 wanasikiliza redio ya ZBC, huku kituo cha Zenj FM ikiwa na asilimia 27.3 ya wasikilizaji, Spice FM asilimia 17.
Kwa upande wa televisheni, kituo cha ZBC kinaangaliwa kwa asilimia 44, wakifuatiwa na TBC yenye watazamaji asilimia 13, Star TV asilimia 11 na ITV asilimia 5.
Kuhusu mtiririko wa vipindi vya ZBC, alieleza kumekuwepo na udhaifu ambapo wakati mwengine vipindi huwa haviruki hewani kwa muda unaotakiwa, ambapo wakati mwengine hulazimika kukatishwa ili kuto nafasi ya vipindi maalum.
Mwafisi alisema katika utafiti huo, wadau wameitaka serikali kuwa na nia ya dhati kuliwezesha ZBC ikiwemo kulifanya kuwa na sheria yake.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk. Omar Dadi Shajak alisema wakati umefika kuondokana na mawazo mgando kuwa vyombo vya habari vimeanzishwa kuisifia serikali iliyopo madarakani.
Alisema serikali imekuwa ikijidhatiti kuutumikia umma iweje chombo cha umma kisiutumikie umma wenyewe.
‘Chombo cha umma kinapaswa kuandaa programu zinazosaidia jamii, programu za mapambano dhidi ya janga la dawa za kulevya, UKIMWI, athari za mabadiliko ya tabia nchi, mazingira’, alisema.
Wakichangia katika utafiti, washiriki wengi walilitaka shirika hilo kubadilika na kufanyakazi kwa mujibu wa mahitaji ya kihabari ya kijamii.
Walisema watu wengine wamekuwa wakikimbia kuvisikiliza vyombo vya shirika hilo, huku wengi wao wakisikiliza vipindi muhimu kama vile matangazo ya vifo.
Kwa upande wake Meneja Utafiti wa Baraza la Habari Tanzania, John Mirenyi aliwataka wanahabari wa Zanzibar wajitokeze wafanye utafiti na baraza hilo litafadhili fedha za kazi hiyo.
Utafiti huo wa Mwaffisi alishirikisha watu 500 wakiwemo wasikilizaji, wafanyakazi na wadau wa habari ambapo umefadhiliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT).
No comments:
Post a Comment