Habari za Punde

Wanafunzi wa Kike Waaswa Kusoma Sayansi

Na Abdi Suleiman, TSJ

WANAFUNZI wa kike kisiwani Pemba, wametakiwa kutoogopa kusoma masomo ya sayansi, ili waweze kuwa wataamu wazuri kwenye kada mbali mbali, ikiwemo udaktari.

Daktari dhamana wa wilaya ya Chake Chake, Dk. Sauda Kassim Omar, huko katika hospitali ya Chake Chake wakati alipokuwa akizungumza na wanafunzi wakike na walimu wao kutoka skuli nane za wilaya ya Micheweni.

Aliwaeleza wanafunzi hao kuwa wakiendelea kuyaogopa masomo ya sayansi hawatopata nafasi za kuwa madaktari wazuri na badala yake watalazimika kutibiwa na madaktari wa kiume.


Dk. Sauda alisema kuwa, wanafunzi hao pindi watakapo jifunza masomo ya sayansi na kuwa madaktari, itakuwa fursa nzuri ya kuwasaidia ndugu na jamaa zao hasa ikizingatiwa kuwa kazi hiyo ni wito.

“Tunahitaji wataalamu wa kada mbali mbali ikiwemo hii ya udaktari lakini hamtaweza kuwa wataalamu wazuri mkiendelea kuyakimbia masomo ya sayansi”,alisema.

Alifahamisha kuwa katika dunia ya sasa huwezi kuepuka masomo ya sayansi kwani mabadiliko yaliyopo yanalamisha watu kubobea kwenye sayansi ili kupiga hatua za maendeleo.

Kwa upande wake muhandisi wa shirika la umeme Pemba, Zakia Juma Azan, aliwataka wanafunzi kushuhulikia masomo yao na kuachana na vishawishi kwa lengo la kufikia malengo yao waliyojiwekeza.

Muhandisi Zakia, alisema kuwa vishawishi vingi watoto wakike hukumbana navyo katika masomo jambo zuri ni kuwa na lengo moja tu kwa kuweka akili zao sawa, watakapo fanya hivyo wataweza kufanikisha malengo yao.

Alisema kuwa, kazi yoyote mwanzo wake ni mgumu, kwani vikwazo vingi mtu hukumbana navyo ikiwemo kwa wanawake kuzarauliwa kwa kutokuweza kufanya kazi kama wanazofanya wanaume,


Naye muwezeshaji wa mradi wa kuwainua wanawake na watoto wakike (WAGE), kutoka shirika la CARE Internatioanl, Chumu Hamad, alisema lengo lao ni kuwainua wanawake na watoto wakike kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Alisema kwamba, mradi huo unategemea hali za wanawake na watoto wakike kubadilika hadi kufikia mwaka 2013, kwa kuweza kusoma na kuandika hususana katika wilaya ya micheweni mkoa wa kusini Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.