WIZARA ya Afya Zanzibar kupitia kitengo cha kupambana na malaria leo kinatarajiwa kuanza zoezi la upigaji dawa majumbani katika wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja.
Akizugumza na Mwandishi wa habari hizi huko Gamba Meneja Mkuu wa kupambana na malaria Zanzibar, Mdungi Khamis Haji alisema zoezi hilo litamalizika Machi 14.
Alisema kuwa lengo la kufanya zoezi hilo ni kutaka kutokomeza malaria wilayani humo na Zanzibar kwa ujumla ili kuhakikisha ugonjwa huo unaondoka hapa nchini.
Aidha alifahamisha kuwa zoezi hilo la upigaji dawa majumbani kwa kipindi kilichopita waliweza kufanikiwa kwa zaidi ya asilimia 90 ndani ya wilaya hiyo.
"Jitihada tumeichukua na tulihakikisha karibuni kijiji kizima walipata huduma hiyo na mwaka huu tutahakikisha kwamba wakaazi wote wa wilaya hii wanapata huduma hii” alisema Mdungi.
Alisema kwa kipindi cha nyuma kuna baadhi ya wananchi walikataa kupigiwa dawa majumbani mwao jambo ambalo linarudisha nyuma ufanisi wa kazi za wizara hiyo.
Nae Msimamizi wa zoezi hilo Haji Mussa Khamis alisema kuwa kuna baadhi ya wananchi walikataa zoezi hilo kwasababu zao za kisiasa na wengine walikosa sababu kwa kusema dawa hizo zina madhara kwa afya ya binadamu.
Hivyo aliwataka wanachi wa wilaya hiyo watoe ushirikiano wa kutosha katika kipindi chote kitakachofanyika zoezi hilo ili kupunguza ugonjwa wa malaria hasa kwa kipindi hichi cha mvua zinazoendelea kunyesha.
No comments:
Post a Comment