Habari za Punde

Madiwani Wahitaji Ushirikiano Usafishaji Mji

Na Hafsa Golo

MADIWANI wa Manispaa ya mji wa Zanzibar wamesema mji huo utaendelea kuwa mchafu pamoja na mambo kuwa holela holela kutokana serikali kuu, kulisusia baraza hilo kwenye majukumu ambayo wakati mwengine chombo kingepaswa kutia mkono wake.

Madiwani hao walieleza hayo jana kwenye mkutano wa kawaida uliofanyika katika ukumbi wa Baraza hilo uliopo Malindi mjini hapa.

Diwani wa wadi ya Amani, Abdalla Ali Chumu alisema Baraza hilo lilipanga kuwahamaisha wanyabiashara kwenye makontena huku hatua zote zikiwa zimekamilika lakini cha kushangaza serikali iliregeza msimamo.


Alifahamisha kuwa kwa hatua iliyofikiwa na Baraza hilo katika kuwahamisha wanayabiashara, serikali ilipaswa kutoa ushirikiano wake kwa asilimia 100 na sio kuregeza msimamo hali ambayo inaendelea kuuweka mji wa Zanzibar katika mazingira ya ovyo.

Diwani huyo alisema kutokana na kadhia ya wafanyabiashara hao, Mkurugenzi wa Baraza hilo alifikia hatua ya kumwagiwa tindikali, huku hivi sasa wakiizingira skuli za Vikokotoni na Darajani ambapo pia wale wa Saateni nao wakitishia kurudi kwenye eneo hilo.

“Hebu itazame serikali imeregeza kamba juu ya suala hili na hadi Mkurugenzi kuathirika, ambapo kwa wakati ule Manispaa ilihitaji ushirikiano wa serikali na sio kurejea nyuma, vipi mji wetu utaendelea kuwa kwenye hali nzuri?”.

Wakizungumzia kadhia nzima ya usafi wa mji huo, madiwani hao walisema wananchi waache kulitishwa lawama Baraza hilo, kwani uwezo iliyonao wa kugharamia usafi wa mji ni mdogo.

Diwani wa wadi ya Karakana Mussa Idrisa, alisema Baraza hilo halipaswi kulaumiwa juu ya usafi kwani lina nyenzo kidogo za kukusanya mapato hali inayopelekea kushindwa kununua vifaa vya kusaidia usafi.

Alisema imefika wakati serikali ikae pamoja na Baraza hilo na iwache tabia ya kuvutana katika utendaji ili waweze kufikia malengo yaliojiwekea katika kuweka mji wa Zanzibar hali ya usafi na iwe kivutio kwa wageni na wakaazi.

Alisema iwapo yatajengwa mashirikiano mazuri kati ya mipango mji, ardhi na Baraza la Manispaa, hivyo uwezekano wa mipango miji itawezekana kupangika na watumiaji wataheshimu taratibu zilizowekwa.

Diwani alisema kufanyabiashara kiholela ni moja wapo ya njia zinazopelekea kuchafua mazingira ya mji hivyo serikali isiwe na huruma katika kuzibiti wale ambao watakuwa wanavunja sheria.

Awali Diwani wa wadi ya Mkunazini ambae pia Mwenyekiti wa kamati ya kazi ujenzi, alisema Baraza la Manispaa pamoja na uhaba wa wafanyakazi litahakikisha kuwa athari za mvua za masika hazitokei katika maeneo ambayo huduma za mitaro ya maji ya mvua zinapatikana.

Alisema upungufu wa wafanyakazi wa kusafisha mitaro yote iliopo mjini yenye jumla ya urefu wa kilomita 27 baada ya kuongeza urefu wa kilomita 16 baada ya mradi wa michirizi awamu ya pili ulipomalizika hivyo kutokana na ongezeko hilo tathmini zinaonesha kila mfanyakazi mmoja wa Manispaa atawajibika kusafisha 600 mita kwa siku.

Aidha alisema mradi wa Huduma za Mjini (ZUSP) Unaofadhiliwa na Benki ya Dunia baada ya kukumilika urefu wa mitaro utaongezeka kutoka kilomita 27 hadi kufikia kilomita 46 kwa hivyo uhusinno wa wafanyakazi wa mitaro yote ni kwa kila mfanyakazi mmoja anatakiwa kusafisha 1,093 mita kwa kila siku.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.