Habari za Punde

Wawakilishi: Utitiri kamati za maendeleo kikwazo

Wapitisha mfuko wa Jimbo kuondoa tatizo

Na Husna Mohammed

WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, wamesema kuwepo kwa utitiri wa kamati za maendeleo katika majimbo na vijiji kunasababisha vikwazo katika ufanikishaji wa mipango na malengo ya jumuia hiyo na kutopata ufanisi.

Wajumbe hao walieleza hayo jana katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi uliopo Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar walipokuwa akichangia mswada wa sheria ya kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo, ambao baadae waliupitisha.

Akitoa mchango wake Mwakilishi wa jimbo la Ziwani, Rashid Seif Suleiman alisema mfuko huo uunganishe kamati za maendeleo ili utitiri wa kamati zilizopo hivi sasa katika majimbo ziondoke.

Alisema wingi wa kamati hizo, imekuwa kikwazo katika kuleta maendeleo ya jamii ambapo kwa kiasi kikubwa malengo na mipango ya kimaendeleo haifikiwi.
iwapo hakutokuwa na upembuzi yakinifu kuhusiana na wingi wa kamati za maendeleo kwa kiasi kikubwa kutaleta vikwazo.

“Kuwepo kamati nyingi za maendeleo kutakwamisha utekelezaji wa mfuko, hivyo ni vyema kuangaliwa upya na upembuzi yakinifu ufanywe”, alisema Mwakilishi huyo.

Aidha aliwataka wajumbe wenziwe wa Baraza hilo kuhakikisha kuwa fedha hizo wanatumia ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuandika ripoti ya matumizi na kupeleka sehemu husika.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kiwani, Hija Hassan Hija alisema uanzishwaji wa mfuko huo ni jambo muafaka kwani utaharakisha maendeleo ya wananchi.

Akitoa mfano alisema nchini Kenya, ambako wana sheria ya mfuko kama huo, wananchi wameweza kupiga hatua za maendeleo kupitia fedha za mfuko kama huo, na kuiomba serikali kuupa ridhaa mfuko huko.

Mapema akiwasilisha mswada huo, waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed alisema serikali imebuni mpango huo ili kuharakisha kazi ya uletaji maendeleo ya wananchi majimboni.

Waziri Aboud, aliwataka wajumbe wa Barza hilo kuzitumia vizuri fedha hizo na kwa malengo yaliyokusudiwa baada ya sheria hiyo kuipitisha rasmi.

Aidha alisema ripoti ya matumizi ya fedha ndio kitu muhimu zaidi kwani itaaninisha maeneo ambayo fedha hizo zimetumika.

Naye Mwanatanga AME, anaripoti kuwa, wajumbe wa Baraza hilo, juzi waliupitisha mswada wa sheria ya Uendeshaji wa Tume ya Mipango Zanzibar na mambo yanayohusiana na hayo, ambapo kupitishwa kwake kunaifuta sheria nambari 5 ya mwaka 1989, ambapo Tume hiyo hivi sasa.

Awali wajumbe wa Baraza hilo walielezea hisia zao za kuwa na shaka ya kuachiwa Rais kuwa ndio Mwenyekiti wa Tume hiyo jambo ambalo waziri huyo alisema hilo haliwezi kuondolewa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango ya Maendeleo alisema ni kutokana na Katiba katika kifungu cha 25 kuelezea kuwa Rais ndie msimamizi wa Tume kwa vile ndio chombo cha juu na itapotokea kumuondoa Rais chombo hicho kitapungua nguvu zake.

Alisema ikiwa Rais ataondolewa ndani ya sheria itasababisha Rais kupewa taarifa kama ni mtu wa pili jambo ambalo haliko sahihi katika utekelezaji wa shughuli za Tume na ndio maana ametakiwa kuwa kiongozi.

Aidha waziri huyo alisema uchumi wowote hauwezi kukua ikiwa kutakosekana kwa mipango ya kitaifa hasa katika suala la utafiti kwa vile ndio eneo muhimu linaloweza kukuza uchumi wa nchi.

Waziri huyo alisema ndio maana hivi sasa serikali imeamua kulipa kipaumbele suala la utafiti baada ya kuunda katika wizara mbali mbali vitengo hivyo ikiwa ni hatua itayowezesha kuleta mabadiliko ya kiuchumi Zanzibar.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.