Na Miza Chande MCC-Maelezo
Kiasi cha tani 3718.8 zenye thamani ya USD 47.8 milioni sawa na Tshs 76,749.1 milion ziliuzwa katika masoko mbali mbali ya kimataifa hasa katika nchi za Indonesi, India, Dubai na Singapore.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Biasha Viwanda na Masoko,Nassor Ahmed Mazrui wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Hoteli ya Bwawani kwa lengo la kuwashukuru wananci kwa kushiriki kikamilifu katika uvunaji wa zao hilo kwa msimu wa mwaka 2011-2012.
Mazrui amaesema uuzaji huo wa Karafuu nje ya nchi ulienda sambamba na uuzaji wa ndani ambapo wakulima wameweza kupata jumla ya Tshs 71,592.2 kutokana na kuiuzia Serikali katika Soko la ndani.
Amesema kati ya Tshs 71,592.2 Jumla ya Tshs 70,228.9 Milioni zilitokana na ununuzi wa Karafuu ambapo Tshs 1,363.3 Milioni zilipatikana kutokana na ununuzi wa Makonyo.
Mazrui amesema Serikali itaendelea kununuwa karafuu kwa bei iliyo tangaza na kutoshusha bei ya kununulia karafuu kwa wakulima hata kama bei itashuka katika soko la dunia.
Amesema kwa hivi sasa hakuna mkulima au mwananchi yeyote ambae anaidai Serikali kupitia Shirika lake la Biashara la Taifa ZSTC kutokana na mauzo ya bei ya karafuu.
Mazrui alisema kuwa pamoja na mafanikio hayo ya karafuu pia serikali haijasita kununuwa makonyo ya karafu na imeweza kununuwa jumla ya tani 909.3 za makonyo na yenye thamani ya Tshs.1,363.3 milioni jambo ambalo limewezesha kiwanda cha mafuta ya makonyo kilichopo hapa nchini kuwa na mali ghafi ya kutosha ili kuzalisha mafuta hayo.
Amesema licha ya msimu huu wa mavuno ya Karafuu kuelekea ukingoni amewaomba wananchi kuendelea kuziuza karafuu zao ZSTC na waachane na mtindo wa kuweka Karafuu majumbani mwao.
Akielezea changamoto ambazo zimejitokeza katika msimu huu wa uvunaji Waziri huyo wa Bishara amesema ni pamoja na ajali za kuanguka ambazo zilisababisha vifo kwa baadhi ya watu ambapo pia amewataka wananchi waliopata matatizo hayo kuwa wastahamilivu na kwamba Serikali imo mbioni kuliangalia suala hilo kulingana na sheria zilizoko.
Katika hatua nyengine amewashukuru wananchi, taasisi binafsi,mashirika ya Kiserikali,vyombo vya habari,Wakuu wa Mikoa, kwa kushirikiana kikamilifu na Serikali jambo ambalo pia limesababisha vitendo vya magendo kupungua kwa kiasi kikubwa.
No comments:
Post a Comment