Habari za Punde

Dk. Bilal: Tunajitahidi Kupambana na Magonjwa ya Binadamu

Na Mustafa Leu, ARUSHA

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilali, amesema serikali imepanua wigo kwa kuweka msukumo zaidi katika utafiti wa magonjwa ya binadamu ili kuweza kuyapunguza na kuyatokomeza.

Dk.Bilal, ameyasema hayo jana alipokuwa akifungua kongamano la watafiti wa Sayansi ulimwenguni, jijini Arusha na kusisitiza kuwa mkakati uliopo ni kuhakikisha utafiti wa magonjwa mbalimbali unafanyika kwa lengo la kuyatokomeza.

Alisema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuzuia vifo vya mama na watoto, sambamba na ugonjwa wa malaria ambao bado ni tishio kwa maisha ya wananchi ili kupunguza vifo hasa kwa wajawazito wanapokuwa wakijifungua.

Alisema changamoto kubwa iliyopo ni kukabiliana na upunguzaji wa magonjwa mbalimbali ya binadamu yanayoambukiza na yasiyoambukiza ili kuyatokomeza.

Awali Mkurugenzi mkuu wa taasisi ya utafiti wa magonjwa nchini Dk. Mwase Malecela, alisema licha ya jitihada zinazofanyika za kuzuia magonjwa bado kuna tatizo la vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano kutokana na kuugua magonjwa mbalimbali.

Alisema wameanzisha vituo katika wilaya za Temeke, na Rungwe,pia katika hospital ya Taifa ya Muhimbili, vya utafiti wa magonjwa yasiyoambukiza vijiji ili kufuatilia na kuangalia maendeleo yake vijijini kuhusu magonjwa hayo.

Ameongeza kuwa NIMR, inakamilisha mchakato wa kufanya kazi pamoja na Hospital ya Ocean road ya jijini Dar es Salaam, kutokana na ongezeko la ugonjwa wa Kansa,ambalo limekuwa ni kubwa mno na linawakumba vijana wengi.

Dk.Mwase, alisema lengo la utafiti ni kuona kama malengo yaliyowekwa yamefikiwa au la na kuona kama bado tatizo la vifo vya watoto chini ya miaka mitano na wajawazito wanaofariki wakati wa kujifungua kama bado ni kubwa kwa kiasi gani..

Alisema idadi kubwa ya vijana nchini sasa wanakumbwa na ugonjwa wa Kansa, ambalo limekuwa ni tatizo kubwa hapa nchini ambapo utafiti utakaofanywa unalenga kupata taarifa na takwimu sahihi za idadi ya walioambukizwa na kasha watazisambaza kwa umma kupitia vyombo vya habari.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.