Na Mwantanga Ame
SPIKA wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, ametoa onyo kali kwa Mawaziri wanaovipiga chenga vikao vya Baraza bila ya sababu na ameitaka serikali kueleza ni kwanini mawaziri wanakwepa kushiriki kwenye vikao vya Baraza hilo.
Mbali na Spika Kificho kuelezea hayo pia ameitaka serikali ifute likizo wanazopewa Mawaziri na Manaibu Mawaziri wakati Baraza hilo likiendelea na vikao vyake.
Kificho alieleza hayo jana asubuhi baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo, Salmin Awadh Salmin, kuwasilisha ripoti ya kamati yake huku baadhi mawaziri walio chini ya kamati hiyo kutokuwepo Barazani.
Kutokuwepo kwa baadhi ya mawaziri walio chini ya kamati hiyo ingekuwa shida kuchukua maelezo sambamba na kutoa ufafanuzi wa hoja za wawakilishi kwenye mjadala wa ripoti ya kamati hiyo.
Kutokana na hali hiyo Mwenyekiti huyo, aliomba kiti cha Spika kuona inawawajibisha viongozi hao kama ilivyofanyika kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano na Ujenzi, Makame Mshimba Mbarouk, ambaye alitakiwa kuliomba radhi Baraza, huku akipewa barua ya onyo.
Wakati hayo yakiendelea, mawaziri waliokuwemo wakati huo ni pamoja na waziri wa Katiba na Sheria Abubakar Khamis Bakary, Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Ramadhan Abdalla Shaaban na Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu, Hamad Masoud.
Wengine ni Waziri ya Afya, Juma Duni Haji, Waziri wa Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto, Zainab Mohammed, Waziri wa Kilimo na Maliasili Suleiman Othman Nyanga, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais fedha Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee.
Wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haji Omar Kheri, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud na Waziri asiyekuwa na Wizara Maalum, Mansoor Yussuf Himid huku Manaibu Mawaziri wakiwa hawamo ndani ya kikao hicho
Kutokana na hali hiyo Baraza hilo lilikosa kuwa na Mawaziri wa baadhi ya Wizara, na Manaibu Mawaziri huku Naibu Waziri wa Afya kutoonekana kutoshiriki kabisa katika kikao hicho tangu kuanza kwake.
Akitoa maelezo yake Spika Kificho, alisema yeye binafsi hafurahishwi na hali hiyo kutokana na umuhimu wa chombo hicho ambacho kilitakiwa kuwa na Wajumbe wenye nidhamu.
Alisema taarifa ambazo yeye anazo ziliwahusu Mawaziri wachache, lakini jambo la kushangaza kuona kuna Mawaziri ambao hawajaonekana katika kikao hicho huku akiwa hana taarifa zao.
Kutokana na hali hiyo Spika Kificho alimtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, kumpeleka taarifa za viongozi hao kwani haelewi ni nani anaowakaimu ili waweze kujibiwa hoja zao.
Kuwepo kwa hali hiyo Spika Kificho, alimtupia mzigo huo waziri Aboud, na Mawaziri waliobakia kujipanga kujibu hoja za kamati hiyo huku akisisitiza lazima vikao hivyo viheshimiwe kwa pande zote.
“Kwa vile vikao hivi msimamizi wa shughuli za serikali ni Makamu wa Pili wa Rais, na yeye amemuachia Kaimu wake waziri wa Makamu wa Pili wa Rais, sasa ningeomba uniletee maelezo Mawaziri hawa wameenda wapi na kwa nini hawajaingia kikaoni”, alisema Spika Kificho.
Alisema jambo la kusikitisha kuona amekuwa na taarifa za viongozi wachache lakini wengi wake hawako ndani ya kikao hicho jambo ambalo linamuiya vigumu kufahamu ni nani anasimamia hoja zao.
Alisema suala la kuheshimu vikao ni moja ya jambo atahakikisha kila mmoja anawajibika nalo kwa kuona haki inatendeka kwa pande zote.
No comments:
Post a Comment