Na Mustafa Leu, ARUSHA
ZAIDI ya watoto 1,500 wenye umri wa wiki 6 hadi 12, wamefanyiwa utafiti wa majaribio ya dawa mpya aina ya RTSS, kwa ajili ya kuwakinga na ugonjwa hatari wa Malaria.
Utafiti huo unafanyika nchi saba barani Afrika ikiwemo Tanzania, ambapo lengo ni kuangalia uwezekano wa kinga hiyo kama itaweza kufaa kutibu na kuzuiana kutokomeza ugonjwa huo nchini.
Mtafiti mwandamizi wa chanjo ya ugonjwa wa malaria, RTSS, kutoka taasisi ya taifa ya utafiti wa magonjwa ya binadamu, NIMRI, Dk. John Lusingi, alieleza hayo alipokuwa akizungumza waandishi wa habari.
Dk. Lusingu, alisema majaribio ya utafiti huo yanaangaliwa kama yataweza kutokomezwa kama ilivyowezekana kwa ugonjwa wa ndui ulitokomezwa mwaka 1978 kwa kutumia chanjo.
Alisema endapo majaribio hayo yataonesha ufanisi shirika la Afya Ulimenguni WHO litaidhinisha matumizi rasmi mwaka 2015 duniani kote ambako maradhi hayo yamekuwa tatizo.
Dk. Lusingu, alisema utafiti huo, unaofadhiliwa na nchi ya Marekani na Ubelgiji, ambapo nchi nyengine mbali ya Tanzania ni Kenya, Msumbiji, Malawi Burkina Faso, Ghana, na Gabon, na lengo lake ni kutokomeza malaria.
Alisema wakati chanjo hiyo ikiendelea kutolewa watoto hao watakuwa chini ya uangalizi wa madaktari ili kuangalia maendeleo na kubaini iwapo kutatokea madhara waweze kuchukua hatua za mapema kuokoa maisha ya watoto yao.
Alisema mpaka sasa kuna mikoa Kagera, Lindi, Mtwara, Kigoma, Pwani na Tanga, bado ina kiwango kikubwa cha maambukizi ya ugonjwa wa malaria, ukilinganisha na mikoa kama Arusha, Manyara, Mbeya na Iringa ,ambayo kiwango cha maambukizi sio kikubwa na hiyo inatokana na mambo kadhaa ikiwemo mazingira,mabadiliko ya tabia nchi, aina za nyumba na uelewa wa wananchi juu ya hatua za kuchukua ili kujikinga na malaria.
No comments:
Post a Comment