Na Aboud Mahmoud
WANANCHI wa Mkokotoni, mkoa wa Kaskazini Unguja, wametakiwa kuwa makini katika kutekeleza mradi wa kuondosha ajira kwa watoto kijijini hapo.
Ushauri huo umetolewa na Mratibu wa mradi huo wa kuondosha tatizo la ajira kwa watoto Zanzibar, Asha Aboud Mzee wakati alipokuwa akizindua kamati hiyo kwa wanakijiji hao.
Mratibu huyo amesema kuanzishwa kwa mradi huo visiwani Zanzibar ni kuwasaidia watoto kujiepukana na ajira hizo ambazo zina madhara kwao na kuendelea na masomo.
Aidha Asha alifahamisha kuwa Jumuiya ya kuhamasisha Maendeleo ya Wanawake Zanzibar (COWPZ) imejipanga kuhakikisha kuwa ina imarisha mradi huo kiutendaji na kutokomeza wimbi la ajira za watoto.
Nae ofisa Mipango wa mradi huo, Shaka Hamdu Shaka alisema tokea mwaka 2004 kwa kushirikiana na wadau mbali mbali COWPZ imekuwa mstari wa mbele kupiga vita ajira za watoto.
Alieleza kuwa shughuli zitakazofanywa na COWPZ ni kuielemisha jamii juu ya athari za ajira kwa watoto, wakiwemo wanajamii wanawake juu ya umuhimu wa elimu kwa watoto wenye umri wa kwenda skuli.
Kamati hiyo ambayo imepewa jina la ‘Kamati ya kupiga vita mazingira magumu na utumikishaji watoto’ ambayo itadumu kwa muda wa miaka mitatu.
Mradi wa kupiga vita ajira kwa watoto ambao ni wa muda wa miaka mitatu umefadhiliwa na Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) kwa kushirikiana na taasisi ya Save the Children ambapo mradi huo utafanyika katika Mkoa wa Kaskazini na Mjini Magharibi Unguja.
No comments:
Post a Comment