Habari za Punde

Vijana Nungwi wataka Hoteli Zichangie Maendeleo ya Jamii

Na Hassan Yahya

VIJANA wa kijiji cha Nungwi wameiomba serikali kuwalazimisha wamiliki wa hoteli za kitalii kijijini hapo kutunia sehemu ya mapato yao katika kusaidia maendeleo ya jamii katika kijiji hicho.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi wananchi hao walisema kuwa inashangaza kuona nungwi sehemu muhimu kwa shughuli za utalii lakini wananchi wake hususani vijana wanakabiliwa na hali ngumu ya maish.

Walisema kuwa wamiliki wa hoteli za kitalii kijijini hapo wanapata faida nyingi lakini bado hawajalenga kuimarisha Nungwi kiuchumi.

Walifahamisha umefika wakati kwa serikali kulivalia njuga suala la wamiliki wa hoteli za kitalii kutowajali wananchi wa maeneo yenye hoteli za wageni.

Walisema pamoja na kutowajali wananchi pia wamiliki wa hoteli hizo hawawapi kipau mbele vijana wazawa wa maeneo hayo katika suala la ajira ndani ya hoteli hizo.

Walisema kisingizio cha wamiliki wa hoteli hizo kuwa vijana wa maeneo hayo hawana elimu inayohusiana na utalii wakati mwenginea haina mashiko kwani zipo sehemu nyengine ambazo unaweza kufanya kazi bila ya kuwa na elimu ya kiwango cha juu.

Jape Silima (27), alifahamisha kuwa iwapo serikali haitatilia mkazo suala hili basi vijana wataendelea kusulubika na maisha wakati sehemu za kutatua matatizo yao zipo.

''Serikali yetu inapaswa kuwasimamia kwa vitendo wamiliki wa hoteli za kitalii ili na sisi wanakijiji tunufaike na rasilimali zetu vyenginevyo tutaendelea kusumbuka na maisha hali ya kuwa sehemu za kutatua matatizo yetu tunazo''alisema Jape.

Kwaupande wao akina mama ya kijiji hicho wamelalamikia tabia ya baadhi ya wafayakazi wanawake wa hoteli za kitalii kujirahisisha kimapenzi kwa waume zao hali inayopelekea mzozo mkubwa katika baadhi ya ndoa wa wanakijiji hao.

Zainab Rashid (38) alisema kuwa tangu kuingia shughuli za kitalii kijijini hapo wanandoa wamekuwa wakitiliana mashaka kutokana na tabia ya baadhi ya wafanyakazi wa hoteli hizo kuingilia kimapenzi ndoa za watu.

''Mungu atusaidie tu lakini utalii umetuletea matatizo makubwa likiwemo hili la kuvunjika kwa baadhi ya ndoa zetu kutokana na umalaya unaofanywa na baadhi ya wafanya kazi wa hoteli za kitalii''alisema Zainab.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.