Habari za Punde

Dk.Shein: Wanaoshindwa Kuwajibika Wang’atuke

Kubembelezana sasa basi

Na Bakari Mussa, Pemba

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema tabia ya kubembelezana kuhusu kuwajibika katika kazi umefikia tamati na sasa kila mmoja atekeleze wajibu wake wa kuwepo kazini na kama akishindwa kufanya hivyo ni bora ajiondowe.

Alieleza kuwa kila mtu ana kazi ya kufanya anapokuwa kazini pake, kwa maana hiyo kila mfanyakazi lazima afanye kazi kinidhamu kwani lengo la Serikali ni kuwahudumia wananchi.

Dk. Shein, alisema hayo jana ukumbi wa Chuo cha Mafunzo ya Amali Vitongoji, Pemba, alipozungumza na Watendaji wa Serikali ya Mkoa wa Kusini Pemba, wakati wa majumuisho ya ziara yake ya kutembelea utekelezaji wa kazi za maendeleo za Mkoa huo, ikiwa ni kukamilisha ziara yake ya wiki moja kisiwani Pemba.

Alifahamisha kuwa ili kuwepo utendaji wa kazi wenye tija ni lazima kila mmoja ajiulize kweli anafanya kazi katika masaa yote anayotakiwa afanye, na kama sio hivyo basi anatumia muda wa Serikali kwa shughuli nyengine ambazo ni zake na hivyo Serikali haitomvumilia.

“Wakati wa kuhimizana kiutendaji mimi leo nasema basi, sitouzungumza tena kwa sababu nimezungumza hayo kwa muda wa mwaka mmoja na miezi minne, kama kuna mtu atazungumza hilo shauri yake mimi basi” alitowa nasaha zake.

Alisema kuwa kila mtendaji ni lazima awe na mpango wa kutekeleza wajibu wake ipasavyo na sio kukaa kitini akisubiri faili zije wakati ziko kazi nyingi za kufanya.

Dk. Shein, alieeza kuwa kila mfanyakazi atapandishwa cheo na mshahara kwa kuzingatia utekelezaji wake wa kazi na sio kugaiwa na lazima ifanyike hivyo ili kuleta maendeleo ya haraka nchini.

“ Aliekuwa hawezi kufanya kazi kinidhamu, zilizowekwa na Serikali aondoke mwenyewe” alibainisha.

Aliendelea kusema kuwa ndani ya Maofisi ya Serikali kuna matatizo, hivyo Watendaji wakuu wawasikilize wafanyakazi wao na matatizo wayaondowe wasisubiri watu wengine waje wayaone.

Alisema ni lazima kuwe na mabadiliko ya kiutendaji ili mafanikio yaweze kupatikana ni lazima kila mfanyakazi aujuwe umuhimu wa kazi.

“ Fanyeni kazi mliyotumwa na wananchi, muache tabia ya kwenda ofisi za wenzenu kupiga soga huo si utendaji mzuri.” alisisitiza Dk. Shein.

Aidha Dk.Shein, alisema kuwa amefurahishwa na taarifa ya Mkoa huo, juu ya maelezo waliyompatia katika utekelezaji wa kazi zao na ameipokea.

Alieleza kuwa amefurahishwa sana na kauli aliyoipata kuhusu amani na utulivu uliopo katika Mkoa huo, jambo ambalo limeletwa na ushirikiano mkubwa baina ya Jeshi la Polisi na Ulinzi Shirikishi jamii,

Aliwapongeza wananchi wa Shehia ya Makombeni, Mkoani Pemba, kwa ushiriki wao mkubwa wa Ulinzi Shirikishi jambo ambalo limemtia moyo na kutaka wananchi wa maeneo mengine kuiga Shehia hiyo.

Dk. Shein, alisema katika ziara yake hiyo aliona mengi katika maagizo aliyotowa katika ziara yake ya mwanzo yametekelezwa na kusema kuwa nia ya Serikali ni kuleta ustawi mzuri wa maisha ya wananchi wake.

Akizungumzia suala la elimu , alieleza kuwa katika Ziara yake hiyo aliridhishwa na maendeleo ya Elimu yaliyopo katika Skuli ya Ukutinni Pemba, kwa ujenzi wa madarasa na kwamba kupatikana kwa madarasa hiyo kutaondowa ufinyu wa nafasi kwa wanafunzi.

Aliwataka wazazi wawatie hamasa watoto kusoma kwa bidii, kwani matatizo yaliyotokea ya kufeli kwa wanafunzi katika mitihani yao yeye binafsi hayakumfurahisha.

Aliendelea kusema kuwa kuanzishwa kwa jengo jengine la Skuli na wananchi wa Ukutini ni hatua nzuri na aliwataka washirikiane na Afisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkoani kuwakumbusha wale waliochukuwa ahadi ya kuchangia wakati wa ziara yake ya mwanzo kufanya hivyo kwani ahadi ni deni.

Alisema ni lazima wananchi wajenge ari ya kujitolea na wasisubiri wafadhili nao watachoka kila siku kutusaidia wafadhili wawe ni wasaidizi tu.

Aliwataka wazazi kuwajibika katika kufuatilia maendeleo ya masomo kwa watoto wao, kwani inaonesha dhahiri kuwa hata wazazi nao hawawajibiki kwa watoto wao kimasomo.

Alisema ni dhahiri kwamba Serikali na Jamii kwa ujumla kukabiliana na tabia ya kuwapa ‘mabomu’ wanafunzi ya kimasomo jambo ambalo ni baya na linaharibu mustakabali wa Taifa na Jamii katika kupambana na Umaskini.

Akizungumzia kuhusu kilimo chaUmwagiliaji maji huko Makombeni, alisema kuwa ameridhishwa na juhudi hizo na ni mategemeo ya Serikali na malengo yake ya kukibadilisha kilimo kilichozoeleka kuwa cha kisasa ili kuongeza tija kwa wakulima.

Alieleza kuwa kwa miundombinu iliyopo hapo ikiwemo maji ya kutosha ni wazi wakulima watalima misimu mingi, hivyo alizitaka taasisi ambazo bado hazijatekeleza wajibu wake katika kukamilisha kilimo hicho kufanya hivyo kwa haraka ili wakulima waweze kulima kilimo hicho.

Hata hivyo alizitaka Taasisi zinazokifanya Kilimo hicho kushirikiana kigharama na wasiiachie mzigo Wizara moja tu, kwani gharama zake kubwa.

Alisema kuwa lengo la Serikali ni kukabiliana na upungufu wa chakula iwe inapunguwa kuagiza Tani nyingi kutoka nje kutoka nusu ya sasa na Serikali imeazimia kuagizia matrekta ya ziada kutokana na wakulima kuhamasika na kilimo katika msimu huu.

Hivyo aliupongeza Mkoa huo kwa kuimarisha kilimo na wawatumie wataalamu wa Kilmo, sasa hivi kazi kubwa ni kilimo na wananchi wameelewa hivyo.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.