Na Joseph Ngilisho, Arusha
TIMU ya Flamingo ya Arusha, juzi iliweka historia ya soka mkoani humo baada ya kunyakua ubingwa wa mkoa bila ya kupoteza hata mchezo mmoja.
Mbali ya kuweka historia hiyo, timu hiyo pia imeweza kutwaa ubingwa huo kabla ya ligi kumalizika hatua ambayo imepongezwa kwa asilimia kubwa na wapenzi wa soka wa mkoa wa Arusha.
Ligi hiyo inatarajiwa kumalizika leo katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid, kwa pambano litakalowakutanisha maafande wa Polisi Longido na Momela.
Katika mchezo wa mwisho juzi, Flamingo ilitoka sare ya bila kufungana na timu ya Nyati ya Mto wa Mbu kutoka wilayani Monduli.
Kwa matokeo hayo, Flamingo imejikusanyia pointi 13, magoli kumi, huku nyavu zake zikitikishwa mara moja.
Timu za Nyati na Arusha Meat, zote zina uwezo wa kufikisha pointi kumi lakini zitalazimika kusubiri hadi mwisho wa ligi hiyo kujua timu itakayoshika nafasi ya pili kulingana na tafauti ya mabao.
Katibu wa timu ya Flamingo Shabani Ally Juma, amewapongeza wachezaji wake kwa kujituma na kuweza kutwaa ubingwa huo bila ya kushindwa hata mchezo mmoja.
No comments:
Post a Comment