Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Jamhuri ya Kiislam ya Iran zimeunda timu ya watu wanne ambao watasimamia upatikanaji wa Mtambo wa kuchapishia magazeti ya Serikali ya Zanzibar ili kuyafanya magazeti hayo kuchapishwa Zanzibar badala ya Dar es Salaam.
Timu hiyo inajumuisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni Utalii na Michezo Zanzibar Dk.Ali Mwinyikai na Mkurugenzi wa Idara ya Makumbusho Dk.Amina ambao watasaidiana na maofisa wawili wa Iran katika kuhakikisha upatikani wa Mtambo huo.
Hatua hiyo imekuja kufuatia ziara ambayo imefanywa na Balozi wa Iran nchini Tanzania Morahhed Ahom wakati alipomtembelea Waziri wa Habari utamaduni Utalii na Michezo Zanzibar Said Ali Mbarouk ofisini kwake Kikwajuni mjini Zanzibar kuzungumzia masuala mbalimbali ya nchi hizo.
Morahhed amesema kwa vile Zanzibar na Iran ni nchi ambazo zina uhusinano wa muda mrefu hivyo kuna kila sababu ya Iran kuisaidia Zanzibar katika mambo ambayo yamo ndani ya uwezo wao.
Miongoni mwa mambo ambayo Iran imeahidi kuyafanyia kazi ni pamoja na kusaidia ukarabati wa magofu ya Zanzibar ambayo yamekuwa kivutio kikubwa kwa watalii kutoka pande zote za dunia.
Kwenye suala la Michezo Morahhed amesema Nchi yake iko tayari kuwapeleka makocha wa mpira wa miguu Iran kupata mafundisho sambamba na kuahidi kuchangia Mipira 100 ya kuanzia katika sekta hiyo.
Aidha ameahidi kutoa nafasi mbili za masomo kwa maofisa wa Zanzibar ambao wataenda kusomea taaluma ya Urithi na Utamaduni katika Jamhuri ya Kiislam ya Iraan
Kwa upande wake Waziri wa Habari,Utamaduni na Michezo Zanzibar Said Ali Mbarouk amemshukuru Balozi huyo kwa ahadi zake na mashirikiano makubwa ambayo yamekuwa yakifanywa na nchi hizo mbili.
Waziri Mbarouk amesema Zanzibar na Iran ni nchi ambazo zina asili na udugu mmoja hivyo kuna kila haja kuendeleza mashirikiano miongoni mwa nchi hizo mbili.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment