Habari za Punde

TURONGE - Matokeo ya Uhakiki wa Mishahara Yasikaliwe

Na Salum Vuai

NI jambo jema kwamba Idara ya Utumishi Serikalini imeona haja ya kufanya uhakiki wa wafanyakazi wake halali ili kudhibiti uwepo wa waajiriwa hewa wanaofisidi fedha za umma kinyume na taratibu.

Kwamba wapo wafanyakazi hewa wanaoendelea kutafuna fedha za nchi bila uhalali, si jambo linalotaka tochi, kwani kama wasingekuwepo, serikali isingeliwaza kuja na zoezi kama hilo.

Kadhia kama hizo zimeshawahi kuripotiwa miaka ya nyuma, na hata kufunguliwa kesi mahakamani baada ya baadhi ya wizara kubainika kuwa wamo madunduvule wanaotafuna mali zisizokuwa zao.

Wafanyakazi hewa hutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kutokufutwa katika orodha ya mishahara waajiriwa wanaofariki na wanaoacha au kuachishwa kazi kwa sababu mbalimbali.

Aidha, wapo baadhi ya waajiriwa halali lakini viwango vya mishahara walipwayo ni batili kutokana na ujanja wanaoutumia kuajiriwa kwa kutumia vyeti feki ambavyo huonesha kuwa wana daraja za juu kielimu ilhali ukweli halisi hauko hivyo.

Sote tumeshuhudia Idara ya Utumishi Serikalini ikichukua hatua ya kulipa mishahara ya mwezi wa Machi katika sehemu za kazi badala ya utaratibu wa sasa wa kuingiziwa kwenye akaunti za benki.

Isitoshe, zoezi hilo ambalo humtaka mlipwaji awasilishe pamoja naye vyeti halisi vya kuhitimu masomo na mafunzo, hufanyika chini ya usimamizi makini wa wahasibu, washika fedha na maofisa kutoka Idara ya Utumishi Serikalini.

Pamoja na uzuri wa zoezi hili, Turonge inapenda kuitanabahisha Serikali juu ya umuhimu wa kutangaza hadharani matokeo yoyote yatakayobainika kufuatia zoezi hilo.

Kutokana na mazingira tafauti, ni hakika wapo baadhi ya wafanyakazi waliokosekana wakati wa kuchukua mishahara yao, pengine kwa kuwepo kwao nje ya nchi kimasomo au kwa shughuli nyengine tafauti.

Ingawa wale wanaosoma au kuwepo likizoni mikoa ya karibu, walihimizwa kuwahi siku mbili za zoezi hilo lililofanyika Machi 27 na 28, mwaka huu, bado ninaamini wapo wengi walioshindwa kuja nchini kwa sababu nilizozitaja hapo juu.

Ninavyoamini, kwa wafanyakazi wenye rikodi safi, hawakuchukizwa na hatua hiyo yenye lengo la kusafisha madoa yanayochafua mfuko wa hazina ya serikali.

Kwa kuwa ninaamini kwamba dema hilo la Idara ya Utumishi Serikalini ni lazima litabaini walipwaji hewa japo wanaojishuku hawatajitokeza kuchukua mishahara hiyo, hapo ndipo pahala pa kuanzia kuhoji sababu ya mishahara hiyo kutokupata wenyewe, ilhali kila mwezi ilikuwa hairudi katika fuko letu la hazina.

Kwa hili la kuwepo wafanyakazi hewa, haliwezi kufanyika kwa mkono wa mtu mmoja, bali kutakuwa na mtandao mpana unaonufaika na 'mradi' huo unaosababisha kuvuja kwa fedha nyingi za umma ambazo zingefaa kuendeshea mambo mengine ya kimaendeleo.

Lakini, tena lakini, zoezi hilo halitakuwa na maana yoyote kama, fedha nyingi za mishahara zitarudi hazina bila kujitokeza watu wa kuzidai pengine kwa kuogopa kubainika ghilba zao kupitia uhakiki huo, na halafu Serikali ikae kimya bila kuweka hadharani hali hiyo.

Kwa kuwa Serikali yetu inaongozwa kwa misingi ya ukweli na uwazi, ninaamini haitafumba macho wala mdomo kwa kukalia ripoti ya kubainika kwa walipwaji hewa au wale wanaolipwa mishahara minono isiyolingana na viwango vyao vya elimu.

Kila siku tumekuwa tukisikitikia hali ngumu ya uchumi, sasa kunapodhihiri kuwepo watu wasiostahiki kulipwa lakini mishahara inaidhinishwa kila mwezi na kusainiwa, huo ndio ule unaoitwa ufisadi ambao wapo wanaodai Zanzibar haupo.

Akili ya mtu wa kawaida, haiwezi kuamini wimbo wa 'Serikali haina fedha', huku kukisikika taarifa za kuhujumiwa rasilimali zake na watu waliopewa dhamana ya kuzilinda kwa manufaa yetu sote.

Bila shaka wananchi watapenda kusikia matokeo ya uhakiki huo, na kujua hatua zitakazochukuliwa dhidi ya wale watakaobainika kuhusika katika kutafuna fedha za umma.

Ni hatua hiyo tu ndiyo itakayolifanya zoezi hilo lionekane la maana, vyenginevyo, tutasubiri miaka michache ijayo kurudia uhakiki huo kwani, bila kuwajibishwa wahusika, mchezo wa mishahara hewa hautamalizika kwani kila siku wafanyakazi wanakufa na wengine kuzikimbia kazi zao.

Tel: 0777 865050
E-mail: salumss@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.