Na Mwantanga Ame
SAKATA la kufutiwa matokeo ya mtihani wanafunzi 3,303 wa kidato nne serikali ya Muungano na serikali ya Zanzibar, imeanza kuwahoji wasimamizi wa mtihani, huo baada ya kuunda kamati huru.
Kuundwa kwa kamati hiyo kunakuja baada ya Baraza la Mitihani Tanzania kuahidi kulifanyia uchunguzi suala hilo katika kikao cha Viongozi wa Baraza hilo na Wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Wanawake na Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi kilichofanyika Mjini Dar es Salaam mwezi uliopita.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani, Joyce Lazaro Ndalichako, katika kikao hicho alisema taasisi hiyo itafanya uchunguzi huo baada ya kubaini huenda wasimamizi wa mitihani walihusika katika udanganyifu uliotokea katika mitihani hiyo.
Ndalichako alisema kinachojionesha uwepo wa uwezekano mkubwa wa wasimamizi kushiriki katika mpango huo kwani haiwezekani ndani ya darasa moja likawa na majibu yaliofanana na inawezekana Msimamizi alishindwa kudhibiti kutembezwa karatasi iliyokuwa na majibu waliokuwa wanapeana wanafunzi hao.
Alisema katika uchunguzi huo pia utawahoji viongozi wa Usalama wa taifa ambao walipewa majukumu ya kusimamia mitihani hiyo tangu kuja kwake Zanzibar.
Alisema wameamua kuwangiza taasisi hiyo kutokana na kuwapo kwa madai ya kuvuja kwa mitihani hiyo jambo ambalo litapaswa kujiridhisha kama kulikuwa na hali hiyo baada ya baadhi ya wazazi kulishutumu Baraza hilo kwamba uzembe haukuwa wanafunzi kuipata mitihani hiyo bali ilitokana na udhibiti mbovu na kusababisha kuvuja.
Aidha, Katibu huyo alisema kwa upande wa wasimamizi wa mitihani katika Mikoa nao pia watahojiwa kutokana na baadhi ya karatasi ya Mtihani wa mwanafunzi wa kujitegemea kukutwa ndani ya nyumba ya mwalimu, baada ya mienzi mitatu baada ya mtihani kufanyika wakati wao wakiwa ni wapokeaji.
Wengine ambao Ndalichako aliwataja ni pamoja na Askari waliokuwa zamu kulinda mitihani hiyo katika skuli mbali mbali kwa vile walishiriki kuwafanyia upekuzi wanafunzi hao wakati wakiingia katika vyumba vya mitihani na haifahamiki kama kazi hiyo waliifanya vyema hadi kuwapo karatasi ambayo ilikuwa na majibu ambayo walipeana wanafunzi hao.
Aidha, Katibu huyo aliwataja wataohojiwa ni pamoja na wanafunzi ambao wameathirika na tukio ili kueleza ukweli msaada walioupata ulitokea wapi na kuweka hadharani walimu waliosababisha kutokea maafa hayo.
Katibu huyo alisema baada ya kamati hiyo kujiridhisha itaweza kutoa matokeo yake mbele ya jamii na haitasita kuona inatoa ushauri kwa serikali kwa vile Baraza la Mitihani la taifa halina Mamlaka ya kuweza kufukuza mtumishi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Mwanaidi Saleh, alithibitisha kuundwa kwa kamati hiyo jana wakati akizungumza na Zanzibar Leo Mjini Zanzibar.
Katibu huyo alisema hivi sasa tayari imeshaanza kazi ya kuwahoji watu hao Kisiwani Pemba ambapo kazi hiyo inaendelea.
Alisema baada ya kumaliza kazi hiyo kisiwani Pemba wachunguzi hao wanatarajiwa kuifanya kazi hiyo kisiwani Unguja ambapo itakutana na makundi tofauti.
Alisema Kamati hiyo imeundwa ikiwa na watu wa pande mbili za Muungano ambapo Zanzibar ina wajumbe wawili ambao ni kamati huru isiyotokana na watendaji wa serikali.
Inakisiwa kuwa kati ya wanafunzi waliofutiwa mitihani hiyo Zanzibar ina wanafunzi zaidi 1200 kati ya 3,303 ambao wamepangiwa kufanya mitihani yao baada ya miaka mitatu.
No comments:
Post a Comment