Habari za Punde

Watendaji Watakiwa Kusimamia Vyema Nidhamu Matumizi ya Fedha za Umma

Na Abdi Shamnah

WATENDAJI wa Wizara, Idara na Taasisi zilizomo katika Wizara ya Habari,Utamaduni, Utalii na Michezo, wametakiwa kusimamia vyema nidhamu, juu ya matumizi ya fedha za umma.

Changamoto hiyo imetolewa jana na Waziri wa Wizara hiyo, Said Ali Mbarouk, wakati alipozungumza na watendaji hao katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Bwawani, ikiwa ni kikao chake cha kwanza tangu ashike madaraka ya kuiongoza Wizara hiyo.


Akizungumza na viongozi hao, Waziri Mbarouk aliwataka watendaji hao kuzielewa ipasavyo sheria zote zinazohusu fedha ili waweze kusimamia kwa ufanisi matumizi ya fedha za Umma katika makusanyo na manunuzi, ikiwa ni hatua ya kuepuka matumizi yasiofaa.

Alisema pale viongozi hao watakapokosa uelewa wa kuzifahamu sheria hizo, watatoa mwanya wa kutokea ubadhirifu, jambo aliloonya kutokulifumbia macho kwa mtendaji yoyote yule atakaesababisha upotevu wa fedha katika idara yake.

Aliagiza kuwepo uwazi katika utaratibu mzima wa matumizi ya fedha pamoja kuwatumia vizuri wakaguzi wa ndani wa hesabu (internal auditor), na kuwataka maofisa hao kufanya kazi zao vizuri ili kuondoa dosari katika Wizara hiyo.

Katika hatua nyingine aliwataka watendaji hao kusimamia nidhamu ya kazi kwa wafanyakazi wao na kusisitiza ulazima wa kufuatwa utaratibu wa kuingia na kutoka kazini pamoja utekelezaji bora wa majukumu ya kazi za kila siku.

Aliwataka watendaji hao kuzingatia umuhimu wa kujiheshimu na kuheshimiana kazini pamoja na kuwataka kutekeleza maagizo yote yanayotolewa bila ya misuguano au kununiana, huku akisitiza umuhimu wa kuweka mbali itikadi za vyama vyao mahala pa kazi.

“Kila mtu hapa ana chama chake, simzui mtu yeyote kujishughulisha na masuala ya kisiasa, lakini wapi na wakati gani ndio suala la kuzingatia, sitamvumilia mtendaji atakaejishughulisha na mambo hayo wakati wa kazi’, alisema.

Aidha aliwataka watendaji hao kujenga mashirikiano kati ya taasisi zao, hatua itakayowawezesha kila kiongozi kufahamu kwa undani masuala ya msingi ya taasisi nyingine.

Mbarouk aliwataka watendaji hao kujituma na kuibua miradi mbali mbali katika kila idara na taasisi zao kwa lengo la kupata fedha ili kuyatafutia ufumbuzi baadhi ya matatizo yanayowakabili badala ya kusubiri ruzuku kutoka Serikalini.

Vile vile alisisitiza haja ya kuzishughulikia kero mbali mbali za wafanyakazi, zikiwemo ile za madai ya maposho kadhaa, mengi kai yake yakiwa yamedumu kwa kipindi kirefu.

Mmoja wa washiriki wa kikao hicho, Amour Vuai, (Mwenyekiti wa BAKIZA) akichangia baada ya maelezo ya Waziri, alimshauri Waziri huyo kusimamia kikamilifu matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili, kwa maelezo kuwa kumekuwepo na upotoshwaji mkubwa wa matumzi ya lugha hiyo unaotokana na mchanganyiko mkubwa wa watu.

Alimshauri Waziri huyo kukaa pamoja na mwenzake wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali,na kufanya upembuzi wa vitabu vyote vilivyoandikwa na waandishi wa Kizanzibari ili vitumike maskulini, kwa lengo la kuepuka matumizi ya vitabu vya Kiswahili kutoka Tanzania BARA, vinavyoaminika kuandikwa kwa lugha isio sahihi.

Wizara ya habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, imeundwa ikiwa na sekta kuu nne za Habari,Utamaduni, Utalii na Michezo na ina jumla ya Idara /Taasisi 18, zikiwemo Kamisheni mbili, Idara nne, Mashirika matatu, Vyuo viwili, Tume moja, Hoteli moja, Mabaraza matatu, Bodi moja na Kituo cha Eacrotanal.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.