Na Mwantangan Ame
WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ramadhan Abdalla Shaaban, amesema Bodi ya Upimaji na Tathmini ya elimu Zanzibar itaandaa mbinu za kupima na kufanya tathmini juu ya uwezo wa kielimu kwa wanafunzi wa Zanzibar.
Waziri Shaaban alieleza hayo jana ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar alipowasilisha Mswada wa kuanzishwa bodi hiyo.
Alisema Bodi hiyo itakuwa na kazi ya kuandaa mbinu za kupima na kufanya tathmini juu ya uwezo wa kielimu kwa wanafunzi wa Zanzibar katika ngazi mbali mbali kwa kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha nne.
Alisema serikali imeamua kuunda bodi hiyo kutokana na mabadiliko ya mfumo wa elimu uliopo, ambao unalazimisha kila mwanafunzi kumaliza kidato cha nne kama elimu ya lazima.
Waziri huyo alisema kutokana na mfumo huo, ni vyema uwepo utaratibu ambao utaweza kupima na kutathmini wanafunzi hao wakati wakiendelea na masomo yao jambo ambalo litasaidia kujulikana mahitaji pamoja na kasoro.
Alisema mfumo uliopo unampima mwanafunzi afikapo darasa la saba na kidato cha pili, jambo ambalo halitoshelezi kwa mfumo wa elimu ya lazima, kwani utakuwa ukimuachia muda mrefu bila ya kupimwa.
Alisema suala la elimu ya lazima haliko katika mambo ya Muungano kwa vile serikali ya Zanzibar ina haki kuunda chombo chake cha kusimamia, kutunga na kutunuku vyeti na stashahada kwa wanafunzi wa ngazi ya elimu ya lazima na mafunzo ya ualimu.
Alisema Bodi hiyo itapoanzishwa itakuwa ni kiungo cha ushirikiano na Baraza la Mitihani la Tanzania na taasisi kama hizo katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na maeneo mengine duniani.
Alisema serikali lazima itekeleze mpango huo kutokana na matakwa ya sera ya elimu ambayo inataka kuandaliwa mpango wa maendeleo ya elimu wa mwaka 2007/2008 hadi 2015/2016.
Alisema utekelezaji mpango huo hivi sasa umeweza kuongeza kwa kiasi kikubwa nafasi za upatikananji wa huduma za elimu ya lazima katika ngazi zote kwani uandikishaji wanafunzi katika ngazi ya elimu ya maandalizi imefikia asilimia 37.1 na elimu ya msingi ni asilimia 118.5.
Wakichangia mswada huo baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walieleza utasaidia kuwaweka wanafunzi katika viwango bora ili waweze kufanya mitihani yao vyema bila ya kujiingiza katika vitendo vya udanganyifu.
Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu, alisema hivi karibuni serikali imejikuta ikipokea vilio vingi vya watu kufutiwa mitihani yao, lakini mswada huo utaweza kuweka mazingira bora wanafunzi.
Nae Mwakkilishi wa Magomeni, Salmin Awadhi, alisema ingawa sheria hiyo kuja kwake inaweza kulipunguza tatizo la aina hiyo, lakini bado Wizara ya Elimu inahitaji kuziangalia adhabu zake kwani zinawaumiza wanafunzi.
Mwakilishi wa Kitope, Makame Mshimba, alisema ipo haja ya baadhi ya vipengele vya sheria hiyo kuangaliwa namna ya uteuzi wa wakurugenzi wanaoteuliwa kusimamia taasisi hiyo ili kusiwe na wasimamizi wasiolingana na fani anayoifanyia kazi.
No comments:
Post a Comment