Makamu wa Rais wa Baraza la Taifa la Jamuhuri ya Cuba Bwana Esteban Lazo Hernandez akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwenye Jumba la Mapinduzi Mjini Havana Cuba.
Nyuma ya Balozi Seif ni Balozi wa Tanzania Nchini Cuba Mheshimiwa Alex Crescent Massinda na nyuma ya Bwana Esteban ni Mkalimali wake Bibi Yeny Echevarria pamoja na baadhi ya Maafisa wa Serikali ya Cuba.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewasili Mjini Havana Nchini Cuba kuendelea na ziara yake ya Kiserikali akitokea Nchini Israel .
Balozi Seif na Ujumbe wake amepokewa na Naibu Waziri wa Mamo ya Nchi za Nje wa Jamuhuri ya Cuba Bwana Marcos Rodrigues Costa pamoja na Maafisa wa Ubalozi wa Tanzania Walioko Nchini humo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi ameambatana na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi, Waziri Ofisi ya Waziri Kiongozi Mh. Mohd Aboud Mohd, Waziri wa Afya Mh. Juma Duni haji, Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya Dr. Malik Abdulla Juma pamoja na baadhi ya Maafisa wa Serikali.
Balozi Seif na Ujumbe wake amekutana kwa mazungumzo na Makamu wa Rais wa Baraza la Taifa la Jamuhuri ya Cuba Bwana Esteban Lazo Hernandez yaliyofanyika katika Jumba la Mapinduzi Mjini Havana.
Bwana Esteban alisema Cuba itaendelea kuwa mshirika wa karibu na Tanzania na Zanzibar kwa ujumla katika harakati za kuwaletea Maendeleo na ustawi wa Jamii Wananchi wa pande hizo mbili.
Bwana Esteban alifahamisha kwamba Mipango itazidi kuimarishwa ili kuona uhusiano wa Kihistoria wa sehemu hizo mbili unakuwa wa kudumu.
Aliipongeza Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar kwa ujumla kwa kuendeleza amani na Demokrasia ambayo ni kielelezo cha kuigwa na Mataifa mengi Duniani na hasa yale ya Bara la Afrika.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Cuba kwa moyo wake wa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika harakati zake za kuimarisha Utawi wa Jamii.
Balozi Seif alisema Msaada wa Cuba kwa Zanzibar umekucha chachu ya kuondokana na matatizo mbali mbali ya Jamii hasa yale ya Sekta ya Afya.
Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Visiwa vya Zanzibar viko mlango wazi katika kuwakaribisha wawekezaji wa Cuba kuwekeza Vitega Uchumi vyao ili kusaidia kunyanyua Uchumi wa Taifa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar pia anatarajiwa kukutana kwa mazungumzo na Waziri wa Afya wa Cuba Bwana Roberto Morales Ojeda pamoja na Waziri wa Biashara za Nje na Uwekezaji wa Nchi hiyo Bwana Rodrigo Malmierca Diaz.
Balozi Seif Ali Iddi na Ujumbe wake atamaliza ziara yake Nchini cuba tarehe 18 Mei na kupitia Nchini Ras al Khaima kwa mualiko wa Mfalme wa Nchi hiyo Bwana Saoud Bin Qasimi. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Ujumbe wake anatarajiwa kurejea Nyumbani Tarehe 22 mwezi Mei mwaka 2012.
Othman Khamis Ame Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
No comments:
Post a Comment