Habari za Punde

Kukacha Kucheza kwa Kikwajuni ... Yazigombanisha Jamhuri, Super Falcon

Na Haji Nassor, Pemba

KUFUATIA ushindi wa Super Falcon wa mabao 5-0 dhidi ya Kikwajuni, timu ya Jamhuri imeibuka na kudai kuwa matokeo hayo yalipangwa ili kuikomoa.

Kwa sababu hiyo, uongozi wa Jamhuri umesema hata kama utashinda katika mechi yake ya mwisho leo kwa kuifunga Kikwajuni mabao mengi na kutwaa ubingwa, haitakuwa tayari kushiriki mashindano yoyote ya kimataifa, ikipinga kitendo hicho.

Jamhuri, imedai kuwa, mchezo huo ulionesha kila dalili kwamba matokeo yake yalipangwa, kitendo kilichoshuhudiwa pia na viongozi wa juu wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), lakini hakikuchukua hatua yoyote licha ya timu hizo kukiuka kanuni za soka.

Akizungumza na Zanzibar Leo kwa njia ya simu, Katibu wa Jamhuri Omar Ahmed, amesema, kilichojitokeza siku ya mchezo huo ni kitendo cha aibu, ambacho kilisababisha baadhi ya watazamaji kuondoka uwanjani kabla ya mchezo kumalizika.

Alieleza kuwa, miongoni mwa wakubwa wa ZFA waliokuwepo uwanjani, ni Makamu wa Rais Pemba, Ali Mohammed, ambao baada ya mchezo walisema wanasubiri ripoti ya Kamishna wa pambano hilo, ambayo hata hivyo, alidai haikueleza chochote juu ya mchezo huo.

Hata hivyo, alieleza kuwa, pamoja na hali hiyo timu yake itakwenda uwanjani leo kwa ajili ya kumaliza ligi dhidi ya Kikwajuni, lakini akasisitiza hata kama watashinda na kuwa mabingwa, hawatarajii kushiriki michuano yoyote ya kimataifa.

Katibu huyo amesema, anaamini mipango hiyo imesukwa na Super Falcon na uongozi wake unazo taarifa zote, pamoja na mipango ya kuishawishi Kikwajuni isiingie uwanjani leo.

Akijibu shutuma hizo, Rais wa Super Falcon Hafidh Suleiman, amezibeza kauli za Jamhuri na kusema timu hiyo imeanza kuchanganyikiwa kutokana na timu yake kuishushia kipigo kizito Kikwajuni, wakijua kwamba hawana uwezo wa kushinda kwa mabao manane leo.

Ameitaka Jamhuri kuacha kuwafuatilia kwani wao hawana ubia wala urafiki wa aina yoyote na Kikwajuni, na kuongeza kuwa kama Jamhuri ilikuwa na lengo la kupanga matokeo ili iwe bingwa msimu huu, haikufanikiwa.

“Pamoja na hayo, sisi hatukuizuia Kikwajuni isiingie uwanjani leo wala kuisafirisha kwani sisi sio tulioileta na hatuna uwezo wa kuiambia chochote kwenye masuala ya soka, kwani kila timu ina uongozi wake”, alibainisha.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa ZFA Ali Mohammed, amesema ripoti ya Kamishna wa mechi ya Super Falcon na Kikwajuni, haikuonesha kama kulikuwa na upangaji wa matokeo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.