Bingwa, zilizoshuka zishajulikana, mechi wakati mmoja
Na Ali Cheupe
KAMA ilivyoanza kwa zengwe Novemba 1, mwaka jana, Ligi Kuu ya soka Zanzibar, inafikia tamati leo katika hali ya mizengwe kama ilivyokuwa wakati ikizinduliwa kiswani Pemba.
Licha ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kupanga mechi za mwisho kuchezwa kwa wakati mmoja, baadhi ya mashabiki wanaielezea hali hiyo kuwa ni sawa na ujanja wa mbuni kuficha kichwa mchangani kutokana na ligi hiyo ilipofikia.
Baadhi ya wadau wamesema, kutokana na kitendo cha timu ya Kikwajuni kugomea mchezo wake na Jamhuri kwa kurejea Unguja, pamoja na ukweli kwamba timu tatu za kushuka daraja zimekwishajulikana, hakukuwa na haja kwa ZFA kung’ang’ania mechi za leo zichezwe kwa wakati sawa kwenye viwanja tafauti.
Aidha, wameeleza kushangazwa kwao na hali hiyo, kwamba katika siku ya kufunga ligi, ni timu nane tu zinazotarajiwa kushuka viwanjani, huku nyengine nne zikiwa zimemaliza mechi zao, tafauti na inavyofanyika dunia nzima.
Wakati Super Falcon imeshajihakikishia taji la ligi hiyo, nazo timu za Kikwajuni, Mundu na maafande wa Polisi, tayari zimeshatoa mkono wa buriani kwa kushuka daraja msimu huu, hata kama zitashinda michezo yao ya leo.
Pazia la ligi hiyo iliyoacha madeni lukuki kwa timu shiriki kutokana na kukosa udhamini, litafungwa kwa mechi kati ya Miembeni SC na Polisi zitakazopeana mkono wa kwaheri kwenye uwanja wa Amaan.
Nao mabaharia wa KMKM wataagana na Mafunzo katika dimba la Mao Dzedong, ambapo Mundu na Chuoni wataagana katika uwanja wa Maungani.
Tayari timu mbili zilizopanda kutoka daraja la kwanza Taifa zimeshafahamika, nazo ni Mtende Rangers, Duma, huku timu ya tatu ikitajariwa kupatikana baada ya michezo kati ya Bandari ya Unguja na Hard Rock yenye maskani yake kisiwani Pemba.
No comments:
Post a Comment