Habari za Punde

Maaskofu Wataka Kukomeshwa Uchomaji Makanisa

Na Mwantanga ame

VIONGOZI wa Makanisa Tanzania wameitaka serikali kuweka mkakati utaokomesha tatizo la utiaji wa moto katika makanisa hautarejea tena ili kuepusha kuzuka kwa migongano ya kidini kati ya waumini wa kikristo na waislamu na Jeshi la Polisi.

Rais wa Maaskofu wa Makanisa ya Afrika Mashariki, na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikan Tanzania, Dk. Valentino Mokiwa, aliyasema hayo jana katika kikao kilichofanyika Ofisi ya Wizara ya Nchi Makamu wa Pili wa Rais Vuga Mjini Zanzibar.

Akizungumza katika mkutano huo Askofu Mokiwa, alisema ingawa hivi sasa vyombo vya ulinzi vimeonesha kushirikiana kutoa msaada wa kudhibiti hali hiyo isiendelee, lakini bado ipo haja kwa serikali ikafikiria zaidi namna ya kulishughulikia hilo kutokana na utaratibu wa sasa wa usalama wa makanisa kuonekana haujazaa matunda.

Alisema hilo linajidhihirisha katika matukio ya utiaji wa makanisa 21 ya Zanzibar yaliyoanza kutiwa moto tangu mwaka 2001 hadi sasa hakuna hata kesi moja iliyowahi kufunguliwa mahakamani.

Hali hiyo alisema haiwapi matumaini kama Jeshi la Polisi limeshindwa kuwatambua wachomaji wa makanisa hayo kwa vile baadhi ya wakati hutokea vitendo vya utupiwaji mawe ndani ya makanisa wakati wakifanya ibada lakini vinaporipotiwa jeshi hilo la Polisi huwapa majibu yasiyoridhisha.

Alisema huo sio utaratibu bora wa kufanya kazi hiyo kiasi ambacho inawapa imani kuwa bado Jeshi hilo lilistahiki kulaumiwa kukuza aina ya vitendo hivyo.

Alieleza hali hiyo imesababisha waumini wa dini hiyo kujikuta wakiwa katika maisha ya ghofu jambo ambalo linahitaji kuangaliwa kwa makini utendaji kazi wa Jeshi hilo.

Alisema hilo ni moja ya jambo la msingi kutokana na hivi sasa kuonekana muda mrefu vitendo hivyo vimekuwa vikiendelea jambo ambalo linaweza kuleta mvurugano wa kidini katika nchi.

“Uoingozi wa makanisa unashukuru kuona Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania na serikali ya Zanzibar kwa kukubali kukaa nao kuzungumzia tatizo lililojitokeza katika vurugu za karibuni, kwani ilikuwa ni kiu yetu kubwa na tunaomba ufikishe salamu hizi kwa Rais kama tulivyosema” Alisema Mokiwa.

Alisema hivi sasa kuna tatizo kubwa la waumini wa dini ya kikiristo kupigwa mawe, kushindwa kufanya biashara ya maduka hata za vinyago, jambo ambali linakera kwani matukio yote yanaripotiwa ndani ya vyombo vya sheria hakuna kinachofanyika.

Alisema kuendelea kuwaita wahuni waliofanya vitendo hivyo hilo sio jambo la kuzingatiwa kwani kinachoonekana yanayofanyika yana mwenyewe na yanaweza kuleta athari kwa jamii ya kikristo.

Alisema kama kuna watu hawataki Muungano kwa waumini wa kikristo kuna taratibu zake za kuchagua sehemu ya kusema mambo hayo, na sio kutumia mihadhara ya kidini kwani kilichokuwa kikiendelea kimeonekana kilipewa kibali cha kufanya shughuli hizo.

Hata hivyo, Askofu huyo alifahamisha ni vyema kwa serikali ikafikiria kuwafanyia uchunguzi wa kina wanaodaiwa kuhusika na mambo hayo kwani kinachotokea sasa hakina uhusiano na mambo ya dini.

“Kanisa limechoshwa wakati mwengine hatuwezi kuachia kama kuna kukashifiana sasa basi tumechoka, tumechoka na tumechoka na tungependa katika mambo ya kidini basi lazima tuwe na muongozo”alisema Askofu Mokiwa.

Alisema ni jambo la kusikitisha hivi sasa kuanza kuwepo kwa kauli za kuwataka watu wa bara kurudi kwao jambo ambalo linaweza likaleta athari kwa pande zote mbili ikiwa litaachiwa kwa vile tayari pande mbili hizo zina mchanganyiko wa watu.

“Ni jambo lisilofurahisha hata kidogo kwani vitendo hivi tusichekee kwani ni kauli za hatari na lazima serikali iwe jabari katika kufanya mambo hayo na sio kuchekeana kwani mivurugano hiyo ya kijamii inaweza kuleta tatizo” alisema Askofu huyo.

“Ukimuona buku katoka kunyoosha vidole basi ujue hilo ni tatizo, kwani tunajua kuna imani za dini hazitanii kwani tunahitaji kusema kusikika sio kuendelea na vitendo hivi” alisisitiza Askofu huyo.

Alisema serikali ya Zanzibar haiwezekani kuwaacha viongozi wa dini kuachiwa kuvuruga amani ya nchi na ni vyema ikafikiria kuona inawawajibisha pale wanapokosea.

Akitoa maelezo yake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed, alisema serikali inakubaliana na dhamira ya viongozi hao kwani inaamini kuwa viongozi wa dini wapo kwa ajili ya kufanya kazi zao kama ni viongozi wa dini kwa kuhakikisha kuwa na elimu ya kutosha ya mambo ya dini.

Alisema inapotokea kwa viongozi wa dini kuanza kuhubiri mambo ya siasa ni sawa na watu wasioielewa dini vyema jambo ambalo serikali italiangalia ili kuepusha mivutano ya kidini.

“Salamu zenu nitahakikisha nnaziwasilisha kwa Rais wa Zanzibar kwa ujumla wake na sitatia langu kwenye nukta basi nitasita lakini sitatia yangu kwani serikali inakerwa sana” alisema Waziri Aboud.

Akiendelea alisema serikali kuvipa uhuru vikundi vya dini kufanya shughuli zao ilitarajia kuwa wangeliweza kufanya vyema kwa kutumia uhuru wa kuabudu lakini ni jambo la kusikitisha hilo halikutokea na wameamua kwenda kinyume na hilo.

Waziri huyo aliwataka viongozi hao wa makanisa kuendelea kushirikiana na serikali ili kuijenga Zanzibar katika mazingira bora ya hapo baadae, kwani kinachoonekana baadhi ya watu wanahubiri dini wasiyoijua na serikali haiwezi kuvumilia mambo hayo yaendelee na watahakikisha sheria za nchi bado zitasimiwa vyema.

Alisema serikali inafahamu kuna watu ambao wanataka kuharibu nchi na wanatumia mwamvuli wa dini kufanya mambo yao jambo ambalo serikali haitakubaliana nalo.

Alisema Serikali katika kulisimamia suala hilo itahakikikisha waumini wote wa dini tofauti inawapa fursa sawa, kwani serikali inafuata mfumo wa serikali isiyo na dini bali watu wake imeruhusu kuwa na dini wanazoziabudu na vitendo vya udhalilishaji, uonevu hilo halitakubali na kila anaetaka kufanya hivyo basi sheria itamchukulia hatua.

Alisema serikali itachukua hatua hiyo kutokana na kujionesha hali kuwa ni tete kiasi ambacho tayari ikiachiwa itaweza kuleta madhara kwani waislamu wa Zanzibar na wakristo ni ndugu.

“Wanaochezea uislamu wa Zanzibar hawana taaluma ya dini hii kwani wanatakiwa kuzungumza mambo ambayo hayaharibu mali ya mtu mwengine kwani mtu mwenye kuhubiri dini vizuri haiwezi kutokea uvunjifu wa amani kwani” alisema Waziri huyo.

Alisema suala la muungano wa Tanzania uliletwa kwa Baraka za Mungu na Rais Karume na Nyerere waliuidhinisha katika karatasi kiasi ambacho kila mmoja ameweza kuwa na uhuru wa kwenda popote ndani ya Tanzania.

Alisema wanaohubiri kutaka kuvunjwa kwa Muungano, waelewe hilo halitawezekana kwani tayari kuna kura zilizowahi kupigwa kuonesha Muungano bado una nguvu Tanzania, na kinachotakiwa ni namna ya vipi Muungno wa Tanzania uwe.

Alisema mataifa ya nje hivi sasa yanahitaji kushirikiana na Tanzania katika masuala ya kiuchumi kutokana na raslimali zilizopo kwani tayari baadhi ya mataifa ya Afrika yameweza kufaidika kuinua uchumi wao ikiwemo Rwanda ambapo Tanzania nayo inaweza kuingia katika kundi hilo ikiwa amani ya nchi haitachezewa.

Wakati huo huo, Msaidizi Mkurugenzi wa Baa ya Mbawala, Catherina Casian, ameitaka serikali kuliangalia Jeshi la Polisi kwa kushindwa kuwapa ushirikiano wafanyabiashara wa sehemu hizo hadi kufikia kuchomewa moto sehemu zao za biashara.

Alisema mmiliki huyo tukio la kubomolewa majengo ya baa hiyo yanawatia wasiwasi mkubwa sana na uhusiano na Jeshi la Polisi, kwa vile walitoa taarifa kwa muda mrefu lakini walikosa ushirikiano hadi baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana.

Alisema inasikitisha kuona wafanyabiashara katika sehemu hizo wamekuwa wakilipa kodi kamili serikalini lakini inashindwa kuwapa ulinzi pale inapotokea kuhitaji msaada na badala yake kujikuta wakiharibiwa mali zao.

Alisema hiyo imekuwa ni jambo la kawaida kwa Jeshi hilo kutokana na watu hao kuelezea hilo kwa muda mrefu lakini hakuna kinachotokea.

“Tunashangaa hawa watu walikuwa wanadai Muungano uvunjike sasa inakuwaje waje kwa Mbawala kwani yeye ndio mwenye hiyo hati ya Muungano, kwanini wasiende kuidai UN au kwa Rais wa Muungano na Rais wa Zanzibar walikusudia maana hapa hawakuvunja kote wamekuja hapa” alisema Mkurugenzi huyo.

Mkurugenzi huyo aliiomba serikali kulifanyia kazi suala hilo kwa kina kwani linaonekana kukusanya viashiria vingi ambavyo haviendami na malengo ya vurugu zilizotokea.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.