Habari za Punde

Watalii Wahakikishiwa Zanzibar ni Shuwari. Vyombo vya Habari Vinapotosha Ukweli .

Na Kunze Mswanyamam DAR ES SALAAM

NAIBU waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu amesema Zanzibar ni sehemu salama kwa utalii tofauti na inavyoelezwa na vyombo vya habari vya kimataifa.

Alisema vyombo hivyo vinajaribu kupotosha hali halisi ili watalii wasiingie visiwani humo, na kwamba haijafikia hatua ya Zanzibar kuwa visiwa visivyotaliika.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Nyalandu alisema machafuko ya Zanzibar yanatofautiana sana na yale yaliyotokea katika badhi ya nchi za kiarabu hadi kufikia watawala kuondoshwa madarakani.

“Serikali inawahakikishia wananchi na jumuiya ya kimataifa kuwa matukio hayo yamepita na haitarajiwa kujitokeza tena kwani zipo jitihada madhubuti zilizowekwa kuhakikisha matukio ya fujo hayajirudii”,alisema Naibu huyo.

Aidha alivitaka vyombo vya habari vya Tanzania kuangalia uzalendo kwanza kabla ya kuamua kuchapisha habari zao kwani wakati mwengine zinaweza kuwatisha wageni na kusabisha kuyumba kwa uchumi.

Akitoa mfano Nyalandu alisema, wakati Kenya ilipata mripuko wa kigaidi wa bomu lakini vyombo vya nchi hiyo havikuandika habari hizo badala yake waliyafanya machafuko ya Zanzibar kuwa ndio ajenda katika vyombo vyao.

Alisema vyombo vya habari vya Kenya vilipuuza mripuko wa bomu wa kigaidi na badala yake kwa maandishi makubwa waliibuka na vichwa vya habari Zanzibar hakukaliki.

Nyalandu alisema sio kwamba vyombo hivyo vya Kenya vilikosea kuandika hivyo bali waliandika makusudi ili kuhakikisha watalii hawaingii visiwani na kuisafisha nchi yao kuwa iko kwenye amani japo mabomu yanaripuka.

Alisema Zanzibar iko kwenye amani na ndio maana kati hayo yanayoitwa machafuko hakuna mtalii ama mgeni aliyejeruhiwa wala kuchomwa moto hoteli za kitalii.

“Nataka niwahakikishie wageni wote kuwa Zanzibar iko salama na msivisikile vyombo vya habari vyenye nia na ajenda walizozipanga”,alisema Nyalandu.

Katika hatua nyingine, Nyalandu alisikitika kwa watalii wanne walioporwa jijini Dar es salaam, akisema kitendo hicho hakina mahusiano yoyote na uharibifu dhidi ya wageni bali ni vitendo ambavyo haviwezi kuepukika hata kwa nchi zilizoendelea.

Wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, watalii wanne waliokuwa wakitembea pembezoni mwa barabra eneo la Masaki, waliporwa vitu mbali mbali ambapo vibaka hao walitumia magari na pikipiki ili kufanikisha uporaji huo.

Alisema tayari polisi kwa kushirikiana na wenye hoteli walizofikia watalii hao, wameweka ulinzi wa kutosha ili kuhakikisha usalama wa wageni wanaofikia kwenye hoteli hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.