Habari za Punde

Mufti Ataka Masheikh Wawafichue Wahalifu

Na Hafsa Golo


MUFTI wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaabi, amewataka masheikh na viongozi wa dini kuwafichua watu waliohosuika na vurugu na ghasia zilizotokea mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mufti Kaabi alieleza hayo jana Ofisini kwake Mazizini mjini Zanzibar kwenye kikao cha mazungumzo kilichozishirikisha taasisi mbali za kidini kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo.

Alisema masheikh lazima wahakikishe wanashirikiana na vyombo vya usalama na kutowaficha waliohusika na uanzishwaji wa vurugu hizo ambazo zilisimamisha shughuli mbali mbali za kijamii.



“Masheikh tuwe pamoja ‘kichangarawe’ kidogo kimepindua treni, hivyo tukiondoe ili tupate nafasi ya kuendelea na safari yetu ya kuwa Zanzibar yenye amani na utulivu”, alisema Mufti huyo.

Alisema uislamu hauruhusu kumficha mhalifu kwani madhara yake yanaweza kuiangamiza jamii nzima na kuhusisha waliokuwemo na wasiokuwemo hali ambayo pia huchangia kutofanyika kwa ibada.

"Masheikh nyinyi ni watu wa hekma na busara na ni viongozi wa dini hivyo tuitumie nafasi ya kusikilizwa na jamii kuleta umoja miongoni mwetu”,alisema.

Akizungumzia lengo kuundwa kwa jumuiya hizo ni kutoa elimu na mafunzo na kuwakumbusha waislamu juu wa wajibu wao wa kumcha Mwenyezi Mungu na kuwakataza kwenda kinyume na makatazo ya dini.

Alibainisha kuwa Uislamu, hauruhusu na hautaki vurugu na fitina miongoni mwa jamii wa chanzo cha fitina na kuchochea vurugu zenye kuleta uvunjifu wa amani.

Naye Sheikh Khalfan Nassor kutoka Jumuiya ya UAMSHO aliyehudhuria kikao hicho, akizungumza na gazeti hili alisema wafuasi wa jumuiya hiyo hawakuhusika na ghasia hizo.

Sheikh huyo alisema waliohusika na uvunjaji wa baa, makanisa na nyumba za kulala wageni ni wahuni na si wafuasi wa UAMSHO.

Alisema hakuna mfuasi wa UAMSHO anayewezaa kudiriki kuvunja baa, kuiba chupa za pombe na kunywa, na kusisitiza kuwa vijana waliofanya hayo ni wahuni.

Mjumbe huyo alisema kuwa pamoja na dhana hizo zilizoshamiri ya kuwa wao ndio walioshiriki kufanya vitendo hivyo suala hilo, halina ukweli kwani hakuna mfuasi hata mmoja katika jumuia hiyo anayekunywa ulevi wa aina yoyote na hivyo hakubaliani na shutuma hizo.

Alisema kuwa polisi ndio chanzo za vurugu hizo baada ya kushindwa kutumia busara katika kumkamata kiongozi wao aliyekuwa msikitini, jambo ambalo lilileta hisia mbaya.

"Nafikiri baadhi ya maofisa wa jeshi la polisi kwa kushindwa kwao kutumia busara ndiko kulikosababisha machafuko haya, waumini walidhani ametekwa”, alisema Sheikh.

Mkutano huo ambao ulizishirikisha jumuiya mbali mbali za kiislamu nchini uliibuka na maazimio kadhaa ambayo yatatumika kama muhimili wa kuendelezwa amani hapa nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.