Habari za Punde

Miche 500 ya Mikarafuu Yapandwa Langoni

Na Rehema Abdulrahman, MCC
MICHE 500 ya karafuu imepandwa katika shamba la Chuo cha Mafunzo Langoni Wilaya ya Magharibi Unguja.

Zoezi la upandwaji wa miche hiyo liliongozwa na Waziri wa Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Mwinyihaji Makame Mwadini, na kutaka miti hiyo iendelezwe kupandwa katika shamba hilo na mashamba mengine ya wananchi.

Alisema zao la karafuu ni uti wa mgongo wa visiwa vya Zanzibar hivyo, halina budi kuenziwa na kupandwa kwa wingi kwa lengo la kuiletea mapato Serikali.

Aidha alisema ili kuweza kudhibiti mabadiliko ya tabia ya nchi ni vizuri kupanda miti ambayo inastahamili ukame wa ardhi kwa ajili ya kurudisha mandhari ya kale na kudhibiti mazingira ya hali ya hewa.

Dk Mwinyihaji, alisema miche hiyo iliyopandwa itunzwe vizuri na kutoa muonekano mzuri katika maeneo hayo, sambamba na kupaliliwa mara kwa mara kwa lengo la kuifanya kuzaa kwa wingi.

Zoezi hilo la upandaji wa miti kitaifa kwa mwaka huu limefanyika katika shamba hilo la Mafunzo lililoko Langoni ambapo lilihudhuriwa na wataalamu na maofisa kutoka idara ya misitu na mali zisizo hamishika Zanzibar, kwa kushirikiana na wapiganaji wa chuo cha Mafunzo Langoni.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.