Uchumi kukua kwa asilimia 7.5
Matumizi ya kawaida yatengewa bilioni 307, 797
Na Mwantanga Ame
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imetangaza kurekebisha viwango vya kodi na ada za huduma mbali mbali ikiwa ni hatua ya kuimarisha mapato ya serikali ambayo inatarajia kukusanya shilingi bilioni 13.3 kutokana na mabadiliko hayo.
Waziri wa Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee, ametangaza hayo jana katika ukumbi wa Baraza la wawakilishi Chukwani nje Kidogo ya Mji wa Zanzibar, wakati akisoma bajeti ya Serikali ya Zanzibar kwa Mwaka wa Fedha 2012/2013.
Waziri huyo alisema serikali imeamua kuongeza baadhi ya kodi pamoja na kutoa misamaha kwa kodi za vyakula ikiwa ni hatua ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya serikali kupitia kodi ambapo kwa mwaka ujao wa fedha inakusudia kutumia kiasi hicho cha fedha
Alisema pato hilo litajumuisha gawio la Shilingi bilioni 2.7 kutoka Mashirika ya Serikali na kuzidisha kupunguza pengo la bajeti kufikia 15.8 bilioni ikiwa ni pamoja na Serikali kutarajia kukopa ndani ili kuziba pengo hilo.
Akizitaja kodi hizo alisema ni pamoja na inayohusu ushuru katika huduma za mahoteli, mikahawa, na kutembeza wageni ambapo kuanzia sasa watalipa asilimia 18 hatua ambayo itaweza kuongeza mapato kufikia shilimgi 1.996 bilioni.
Alisema serikali inachukua hatua hiyo ikiwa ni sehemu ya kuona walipa kodi wanakwenda sambamba baada ya kujitokeza malalamiko katika ulipaji wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT), ambapo wafanyabiashara waliosajiliwa kulazimika kulipa asilimia 18 huku wenye mahoteli wakiwa wanalipia kodi hiyo kwa asilimia 15.
Kodi nyengine ambayo imetajwa kuangaliwa na serikali katika bajeti ijayo ni ushuru wa Stempu ambapo inapendekeza kuweka ukomo wa kiwango cha juu cha kutoza ushuru wa stempu katika mikopo.
Hatua hiyo Waziri huyo alisema serikali haikusudii kuongeza mapato bali itasaidia kushajiisha Uwekezaji, biashara na kuiwezesha Zanzibar kumudu ushindani na usawa wa kodi miongoni mwa wakopaji.
Ushuru mwengine ambao serikali imeamua kuirekebisha ni kodi ya kiwango cha ushuru wa stempu kwa biashara ambazo zilikuwa ni asilimia moja na nusu kwa mauzo yanayoanzia shilingi 1,000 ambapo kuanzia sasa kodi hiyo itakuwa ni asilimia tatu ambayo itawezesha serikali kukusanya shilingi bilioni 2.10.
Vile vile Waziri huyo alitangaza kuongezwa kwa ada ya Bandari ambapo kwa sasa abiria wanaosafiri baina ya zanzibar na Tanzania Bara kutoka shilingi 1000 ya sasa hadi shilingi 2,000 huku wataokwenda Pemba watatozwa shilingi 1000 kwa wanaotoka Unguja.
Hatua hiyo alisema itasaidia kuiingizia serikali shilingi 2.00 bilioni ambapo fedha hizo baada ya kukusanywa zitatumika kwa ajili ya kununulia madawati kwa ajili ya skuli za Zanzibar.
Kodi nyengine ambayo serikali imeitangaza kuipandisha ni kodi inayohusu ushuru wa mafuta ya nishati ambapo kwa kila lita hivi sasa inayoingia hapa kwa kutozwa kodi ya shilingi 50 ambayo itawezesha serikali kukusanya shilingi bilioni 3.3.
Waziri huyo pia alisema kodi nyengine ambayo itarekebishwa ni pamoja na ya usafiri barabarani ambapo kuanzia sasa serikali itarekebisha leseni za njia.
Alisema serikali kwa mwaka ujao wa fedha inapendekezwa kurekebisha kiwango cha leseni za njia ili kiendane na uzito wa gari au na ukubwa wa injini yake na hatua hiyo inatarajiwa kuiingizia Serikali jumla ya shilingi 2.1 bilioni.
Waziri huyo pia alisema, idadi ya magari nchini inaongezeka kila mwaka na hivyo kuathiri mazingira kutokana na moshi unaotoka katika magari hayo na serikali inapaswa kuchukua hatua zaidi za kukabiliana na athari za uharibifu huo ikiwemo gharama za matibabu.
Alisema kwa mwaka ujao wa fedha, inapendekezwa kutozwa shilingi 15,000 kwa kila gari kwa mwaka na shilingi 3,000 kwa chombo cha moto cha magurudumu mawili au matatu na hatua hiyo inatarajiwa kuingizia serikali shilingi 700 milioni.
Aidha, Waziri huyo alisema Serikali inakusudia kutumia asilimia 80 ya fedha hizo, sawa na shilingi 560 milioni, kama ziada katika ununuzi wa dawa kwa ajili ya hospitali za Zanzibar, wakati asilimia 20 iliyobaki sawa na shilingi 140 milioni zitatumika kugharamia upandaji wa miti katika maeneo yaliyoharibiwa kimazingira.
Aidha, Waziri huyo ametangaza kuondolewa kwa msamaha wa kodi ya mapato katika miradi mipya ya kibiashara katika maeneo huru ya Uwekezaji na Bandari Huru na kodi hiyo haitahusisha kwa miradi ambayo tayari imeidhinishwa na inaendelea kufanya kazi hapa nchini.
Hatua hiyo alisema inakusudia kuimarisha sekta ya uwekezaji katika maeneo ya viwanda na kijiografia katika kisiwa cha Pemba.
Waziri huyo pia alitangaza kufanyiwa mabadiliko ya kodi zinazohusu wafanyakazi wageni wanaoletwa kama wataalamu baada ya kubaini kuwepo kwa udanganyifu unaofanywa na watendaji hao.
Alisema kazi hiyo serikali itaifanya kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapto Tanzania (TRA), ZIPA na Idara ya Uhamiaji Zanzibar ambayo itaenda sambamba na kuziangalia ajira ambazo hazina ulazima kushikwa na Wazanzibari.
Alisema pia itaziangalia ada za Serikali inazozitoa kwa huduma zake mbalimbali katika Wizara, Idara na Taasisi zake baada ya kusikiliza malalamiko ya muda mrefu ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ambao waliomba kuangaliwa baada ya kuona viwango vya ada hizo vimepitwa na wakati na vinahitaji kufanyiwa mapitio na kurekebishwa.
Alisema Serikali itafanyia mapitio hayo kwa Sheria na Kanuni zake na kurekebisha Ada hizo hatua hiyo ambayo inatarajiwa kuiingizia Serikali jumla ya shilingi 0.5 bilioni.
Waziri huyo alisema pia serikali kutokana na mapitio
ya kiwango cha mauzo ambacho mfanyabiashara hatofikia kiwango inapendekeza kupandisha kiwango cha mauzo ambacho mfanyabiashara hatosajiliwa kwenye VAT kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 15 milioni kwa mwaka hadi kiwango cha mauzo ya shilingi 30 milioni.
Alisema pamoja na mafanikio yaliyopatikana, changamoto kubwa inayoikabili sekta ya afya ni idadi kubwa ya vifo vya mama na watoto na Serikali imeamua kuchukua hatua maalum za kukabiliana na hali hiyo kwa kuondoa ada ya uzazi.
"Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na malalamiko kutokana na hatua ya Serikali kutoza fedha kutoka kwa akinamama ili kuchangia huduma za kujifungua hali yetu ya fedha sasa imeimarika kiasi na hivyo Serikali inaweza kubeba jukumu hili bila ya kuathiri ubora wa huduma" alisema Waziri huyo.
"Kama mtakavyokumbuka, wakati akiwa katika ziara Mkoa wa Kusini Unguja mnamo tarehe 9 Mei mwaka huu, Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein aliagiza kusitishwa kwa tozo hilo kwa akinamama. Nina furaha kulijuulisha Baraza lako tukufu kuwa utekelezaji wa agizo hilo la Mheshimiwa Rais utaanza rasmi tarehe 1 Julai, 2012 na hivyo akinamama wanaojifungua katika hospitali za Serikali hawatachangia tena na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itagharamia gharama za kujifungua kwa akinamama hao" alisema Waziri huyo.
Akizungumzia juu ya huduma ambazo serikali imeamua kuzipa kipaumbele alisema kwa mwaka ujao ni pamoja na kuimarisha sekta ya afya na pamoja na kuendelea na zoezi la mfumo wa kupeleka dawa kulingana na mahitaji halisi ya kituo, ambapo vituo 19 vimo katika Mpango huo wa majaribio.
Aidha, alisema hospitali kuu ya Mnazimmoja inaendelea kushirikiana na madaktari wa nje mbali mbali kuendesha kambi za operesheni na katika kipindi cha miezi tisa cha Julai 2011 hadi Machi 2012, jumla ya wagonjwa 822 wamefanyiwa uchunguzi na kati yao wagonjwa 199 walifanyiwa upasuaji na Serikali kuokoa jumla ya dola za Kimarekani 1.6 milioni kama wangesafirishwa nje ya nchi.
Waziri huyo pia alieleza kuwa serikali katika kipindi hicho imeweza kununua mashine mbili za kuhifadhia dawa za chanjo kwa ajili ya chanjo mpya ya kuzuia maradhi ya kuharisha pamoja na vifaa mbali mbali vya chumba cha wagonjwa mahtuti (ICU) huku ujenzi wa bohari kuu ya dawa unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni 2012.
Akizungumzia kipaumbele chengine, Waziri huyo alisema kitahusu sekta ya elimu ambapo jumla ya madarasa 80 kati ya 200 ya skuli za msingi yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi yamekamilika na kuanza kutumika Unguja na Pemba.
Aidha, alisema jumla ya madawati 500 kwa skuli za msingi yamechongwa na kusambazwa katika skuli za Unguja na Pemba na skuli mpya tatu za sekondari zimekamilika na nyengine tisa ziko katika hatua za kukamilishwa mpango ambao umeenda sambamba na walimu 186 wameajiriwa katika skuli mbali mbali Unguja na Pemba.
Sekta nyengine ambayo serikali itaiangalia alisema ni ya upatikanaji wa maji safi na salama ambapo serikali itachimba visima vitatu katika maeneo ya Chumbuni, Kituo Kikuu Saateni kwa ajili ya kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa huduma ya maji katika Mkoa wa Mjini Magharibi ambao tayari umekamilika.
Aidha, waziri huyo alisema kazi za ulazaji wa mabomba mapya imefanyika kwa maeneo ya Kinuni, Kijichi, Magomeni, Mpendae, Chuini na Kihinani na kwa upande wa Pemba uchimbaji wa visima, Ujenzi wa vituo, Ujenzi wa ‘wellhead’ pamoja na upelekaji wa umeme umekamilika kwa maeneo ya Chokocho, Michenzani, Junguni na Konde.
Pia Waziri huyo alisema kwa upande wa miundombinu ya umwagiliaji, msingi mkubwa wa mita 670 na msingi wa ndani wa udongo wa mita 150 katika bonde la Bumbwisudi; mtaro wa saruji wa mita 200 katika bonde la Makombeni Pemba na mita 525 Kianga imejengwa.
Waziri huyo pia alisema ujenzi wa barabara ya kifusi mita 100 umefanyika Bumbwisudi na tani 1090 za mbolea aina ya TSP 545 na Urea zimenunuliwa na kusambazwa kwa wakulima.
Waziri huyo alisema Serikali imeendeleza juhudi za kuimarisha kilimo cha mpunga wa NERICA baada ya majaribio ya mbegu hii kuonesha mafanikio katika kipindi cha Julai 2011 hadi Machi 2012, ambapo jumla ya tani 21 za mbegu zilizalishwa na kusambazwa kwa wakulima na wazalishaji mbegu.
Aidha, mashamba ya mfano wa uzalishaji alisema yamefanywa kwa shehia 230 Unguja na Pemba ili wananchi wapate kujifunza njia bora za ukulima na upandaji wa NERICA mpanho ambao umeenda sambamba mabwana shamba 183 na maafisa wilaya 18 pia wamepewa mafunzo hayo.
Akizungumzia hali ya uchumi wa Zanzibar kwa mwaka 2012 unatarajiwa kuimarika zaidi kwa kutekeleza malengo ya uchumi na unatarajiwa kwenda sambamba na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2020, MKUZA II, Malengo ya Milenia pamoja na Mageuzi ya Msingi.
Alisema kwa mwaka 2012, uchumi wa Zanzibar unatarajiwa kukua kwa asilimia 7.5 kutoka ukuaji wa asilimia 6.8 mwaka 2011. Matarajio ya ukuaji wa uchumi kwa mwaka 2012 yanatokana na mambo tofauti ikiwa pamoja kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya biashara hasa zao la karafuu.
Maeneo mengine aliyataja ni pamoja na kuongezeka kwa uwekezaji binafsi ikiwa pamoja na miradi ya uvuvi wa bahari kuu, kilimo na miradi ya utalii., kuongezeka kwa uingiaji wa watalii nchini kutokana na hatua mbali mbali zinazoendelea kuchukuliwa na taasisi mbali mbali za kuutangaza utalii wa Zanzibar.
Alisema lengo ni utalii kwa wote, ambao utatuwezesha kila mmoja kuweza kushiriki katika kuutangaza utalii wa Zanzibar huku serikali ikitarajia kukamilika kwa uwekaji wa waya wa umeme wa chini ya bahari kutoka Rasi Kiromoni ya Tanzania Bara hadi Rasi ya Fumba.
Alisema ukamilikaji wa zoezi hilo utawezesha upatinakaji wa umeme wa uhakika katika kisiwa cha Unguja ambapo utasaidia kushajihisha maendeleo ya kiuchumi na utekelezaji wa Program ya Mageuzi ya Kilimo Zanzibar, ambayo itashajiisha uzalishaji na kuongeza tija na kuhakikisha uhakika wa chakula.
Vile vile alisema kuimarika zaidi kwa mashirikiano baina ya sekta za umma na binafsi ambapo inatarajiwa kuwa ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi wa Zanzibar.
Alisema hatua hiyo inatarajiwa kuingiza shilingi 700 milioni na serikali inakusudia kutumia asilimia 80 ya fedha hizo, sawa na shilingi 560 milioni, kama ziada katika ununuzi wa dawa kwa ajili ya hospitali wakati asilimia 20 iliyobaki sawa na shilingi 140 milioni zitatumika kugharamia upandaji wa miti katika maeneo yaliyoharibiwa kimazingira.
Alisema serikali inakusudia kutumia asilimia 80 ya fedha hizo, zitazotokana na kodi ya sawa na shilingi 560 milioni, kama ziada katika ununuzi wa dawa kwa ajili ya hospitali za Zanzibar wakati asilimia 20 iliyobaki sawa na shilingi 140 milioni zitatumika kugharamia upandaji wa miti katika maeneo yaliyoharibiwa kimazingira.
Waziri huyo aliiomba serikali kuidhinishia shilingi bilioni 648.9 kwa mwaka wa fedha 2012/2013. pamoja na kukusanya jumla ya shilingi bilioni 648,944 milioni pamoja na matumizi ya shilingi 307,797 milioni kwa kazi za kawaida na shilingi 341,147 milioni kwa kazi za maendeleo.
Viongozi mbali mbali wa serikali walishiriki katika usikilizaji wa bajeti hiyo akiwemoWaziri Kiongozi Mstaafu, Ramadhan Haji, Mke wa Makamu wa Pili wa Rais Mama Asha Seif Iddi, mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao Zanzibar na Viongozi wa Vikosi Maalum na taasisi za kifedha na taasisi za kitaifa na kimataifa.
Viongozi wengine ambao walishiriki katika bajeti hiyo ni pamoja na viongozi wa Vyama vya kisiasa, Mkuu wa Sheikh Ali Yousuf, makatibu Wakuu wa Serikali ya Zanzibar, Watendaji wa Mashirika ya Kimataifa na viongozi wa dini.
Wajumbe wa baraza la wawakilishi wanatarajiwa kuanza kuijadili bajeti hiyo kuanzia Jumatatu ya wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment