Habari za Punde

Maalim Seif: Hatutawasaliti Wazanzibari. Ataka Wananchi Watoe Maoni ya Katiba kwa Amani, Kustahmiliana.

Na Mwashamba Juma
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, amewatoa hofu Wazanzibari akiwaeleza kuwa viongozi wa SMZ ni wazalendo, wenye kujali maslahi ya Zanzibar na kwamwe hawatawasiliti katika suala la mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Maalim Seif alisema viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wapo kwa ajili ya kulinda maslahi ya wananchi, kwa sababu wameingia madarakani kutokana na ridhaa zao, hivyo wasiwe na hofu juu ya suala la kulindwa maslahi ya Zanzibar, wakati wa mchakato huo.

Maalim Seif, alieleza hayo jana alipokuwa akifungua kongamano lililoandaliwa na Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC) kwa kushirikiana na Ford Foundation, kujadili Muungano na mchakato wa Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lililofanyika katika ukumbi wa EACROTANAL mjini Zanzibar.

“Naomba kuchukua nafasi hii kuwatoa wasiwasi wananchi hasa Wazanzibar, viongozi wao wametokana na Wazanzibari, ni Wazanzibari kindakindaki, wenye kujawa na uzalendo, wanaoipenda Zanzibar..., kamwe hawatawasaliti”, alisema Maalim Seif.

Alisema serikali yao itaheshimu na kutetea maoni yatakayotolewa na wananchi kwa tume ya Jaji Warioba ya kukusanya maoni juu yamabadiliko hayo ya katiba.

Hata hivyo alitumia fursa hiyo, kuonya Wazanzibari wasijefanya kosa la kutokwenda kutoa maoni yao wakati Tume hiyo itakapopita maeneo mbali mbali wakikusanya maoni.

Alisema endapo watashindwa kujitokeza kutoa maoni yao wakati Tume hiyo itakapopita kutoa maoni na mchakato ukimalizika bila ya maoni yao kuchukuliwa na kuchukuliwa ya wengi wenyewe ndio watapaswa kujilaumu.

Akizungumzia Muungano na mabadiliko ya Katiba, Maalim Seif alisema si haki kwa Wazanzibari kuzuiwa kuujadili Muungano wa Tanzania, katika mabadiliko hayo ya Katiba.

Aliwaeleza washiriki wa Kongamano hilo kuwa, Kwa Wazanzibari ambao tayari wanayo Katiba yao, jambo muhimu kwao katika mchakato mzima wa mabadiliko ya Katiba ni suala la Muungano, hivyo waachwe waujadili kwa kina.

Hata hivyo Maalim Seif alisisitiza kuwepo amani, utulivu na kustahmiliana katika utoaji wa mawazo, ambapo kila mmoja ajisikie huru na kila mmoja aheshimu mawazo ya mwenzake.

Aidha alisema katika mchakato huo jambo muhimu la kuzingatiwa ni mawazo ya wengi kuheshimiwa na ya wachache kuheshimika kwa mizania iliyo sawa.

Akiwasilisha mada ya Muungano na Mchakato wa Katiba, Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar Ibrahim Mzee Ibrahim alisema katika mchakato mzima wa marekebisho ya katiba suala la msingi ni kuzingatia haki na Demokrasia kwa maslahi ya Watanzania wote.

Wakichangia mada ya Muungano na mchakato wa Katiba katika kongamano hilo, baadhi ya washiriki walisema elimu ya uraia inahitajika kwa Wazanzibari kwani walio wengi hawaijui katiba wala vipengele vyake hivyo ni vyema kufahamishwa ili wawe na ushiriki mzuri wakati wa kutoa maoni yao.

Mmoja wa washiriki hao kutoka ZAPHA+ Consolata John, alisema wananchi wasaidiwe kujua mapungufu ya Muungano, iliwapate kutoa maoni yao juu ya marekebisho ya mapungufu hayo kwa kuepuka kutafarakiana baina yaou, alisema Muungano huu umebarikiwa na Mungu, kwani Watanzania tayari wamechanganya damu.

"Muungano huu umebarikiwa na Mungu, kama si Mzanzibari kamuoa Mtanganyika na kupata watoto ama Mtanganyika kaoa Mzanzibari, sasa hawa watoto tutawapeleka wapi? alihoji Consolata.

"Nasema hivi kama mwanamke kwani kila penye kuunga au kuvunja Muungano lazima patokee umwagaji wa damu, na katika hili wanawake na watoto ndio waathirika wakuu" aliendelea kuchangia kwa masikitiko.

Nae Mbaraka Said Soud kutoka Wizara ya Utumishi wa Umma Zanzibar alisema kuvunjika kwa Muungano haimaanishi kuvunjwa ama kugawanwa kwa familia, bali zinaungwa ni serikali na kugawana mamlaka kwa kupewa kila moja na mamlaka yake na familia kuendelea kama zilivyo.

"Bora tuwe na ujirani mwema wa kusaidiana na kupendana kuliko kuwa na udugu wa kudhulumiana", alisema mmoja wa washiriki hao.

Akifunga Semina hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya ZLSC, Profesa Chris Maina Peter, aliwataka washiriki na wananchi wote kutoa maoni yao kama wanavyoona inafaa, kwani huko ni kutumia haki yao ya msingi kisheria.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.