Habari za Punde

Bihindi: Ni ndoto kurejesha ligi ya Muungano

Na Mwantanga Ame

SERIKALI ya Zanzibar imesema ni ndoto ya mchana kurejesha ligi ya Muungano, hasa baada ya Zanzibar kupata uanachama shirikishi wa Shirikisho wa Soka Afrika (CAF) unaoiwezesha kushiriki mashindano ya klabu barani humo.

Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni Utalii na Michezo, Bihindi Hamad Khamis, amesema hayo jana wakati akijibu suala la Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni Jaku Hashim Ayoub, aliyeuliza sababu ya lengo la Zanzibar kujiunga FIFA halijafikiwa na ni lini serikali itarejesha ligi kuu ya Muungano.

Bihindi alisema suala la kurejesha ligi kuu ya Muungano kwa sasa halipo, kwani ligi hiyo ilikuwa na lengo la kutafuta wawakilishi kwenye mashindano ya klabu barani Afrika, nafasi ambayo sasa Zanzibar imeipata.

Aidha, amesema serikali haifanyi jitihada zozote kutoa msukumo wa kuzifanyia marekebisho katiba za Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) na TFF, kwa lengo la kuwaingiza wajumbe wa Zanzibar ndani ya TFF ili kuleta sura ya Muungano.

“Serikali haioni haja ya kufanya hivyo kwani michezo si jambo la Muungano na Zanzibar inaendeshea shughuli za kimichezo kwa kujitegemea yenyewe”, alisema Bihindi.

Akifafanua, alieleza kuwa, iwapo ligi hiyo itarejeshwa tena kwa madhumuni yale yake ya kupata timu za kuiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya CAF, huenda ikapunguza nafasi ya Zanzibar kwani washindi wanaweza kupatikana kutoka upande wowote bila kuzingatia uwiano wa nafasi.

Hata hivyo, Naibu Waziri huyo alisema serikali kupitia Kamisheni ya Michezo na Utamaduni, imekuwa ikichukua jitihada mbalimbali kuhakikisha inafufua hamasa ya mchezo huo kwa pande hizo kuanzisha mashindano mbalimbali ya pamoja.

Ametoa mfano wa Kombe la Mapinduzi na lile la Urafiki linaloshirikisha pia timu kutoka nchini Misri.

Bihindi amesema wizara yake itajitahidi kuwasiliana na wenzao wa Bara kwa ajili ya kubuni na kuweka utaratibu utakaoinufaisha Zanzibar na misaada ya FIFA ikiwemo vifaa na mafunzo ya makocha na waamuzi ambayo hupitia TFF.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.